Makete, 17 Machi 2025
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Dkt. David Mathayo David, akiambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), leo imeendelea na ziara yake mkoani Njombe kwa kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Makete.
Katika ziara hiyo, Kamati ilitembelea kijiji cha Mang’oto, Tarafa ya Mang’oto, wilayani Makete na kutoa pongezi kwa REA kwa kusimamia vyema mradi huo na kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya nishati ya umeme.
Akizungumza baada ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Dkt. David Mathayo David, amepongeza REA kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kusambaza umeme vijijini, huku akitoa wito kwa mkandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha maeneo yote yaliyopangwa yanafikiwa kwa wakati.
“Tunawapongeza REA kwa kazi nzuri ya kusimamia miradi ya umeme vijijini, hususan hapa Mang’oto. Hata hivyo, tunamtaka mkandarasi kuongeza kasi ili maeneo yote yaliyobaki yaunganishwe haraka na wananchi waweze kunufaika na huduma hii muhimu,” alisema Dkt. Mathayo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kutatua changamoto zote za umeme nchini na kuhakikisha vitongoji vyote vinapatiwa nishati ya umeme ili kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha uchumi wa wananchi.
“Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kila kijiji na kitongoji kinapata huduma ya umeme. Lengo letu ni kurahisisha utoaji wa huduma muhimu kama afya na elimu, pamoja na kuwezesha wananchi kufanya biashara zao usiku na mchana bila vikwazo,” alisema Mhe. Kapinga.
Naye Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Jones Olotu, alisema kuwa serikali imejipanga kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme vijijini, ambapo katika siku za hivi karibuni wanatarajia kutangaza tenda nyingine ili kuongeza nguvu katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Tunatambua kuwa umeme ni kichocheo muhimu cha maendeleo kwa wananchi wetu. Kwa kutambua hilo, hivi karibuni tutatangaza tenda nyingine ili kuongeza nguvu katika usambazaji wa umeme kwenye vitongoji vilivyobaki na kuhakikisha maeneo yote yaliyopangwa yanafikiwa kwa wakati,” alisema Mhandisi Olotu.
Mkazi wa Mang’oto, Bw. Daniel Mbilinyi, alieleza furaha yake kwa kupata huduma ya umeme kupitia mradi wa REA, akisema kuwa umeme huo umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao, hususan katika shughuli za uzalishaji na biashara. Pia, alituma salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wa vijijini.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Bunge pia ilifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo, ambapo walipata fursa ya kutoa maoni yao kuhusu miradi ya umeme na maendeleo kwa ujumla.