MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Machi 17,2025 jijini Dodoma kuhusuzoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura lililoanza leo katika Mkoa wa Dar es Salaam .
Na.Alex Sonna-DODOMA
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila,amewaonya watu wanaopotosha mtandaoni kwa kuhamasisha wananchi wasijitokeze katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
RC Chalamila ametoa onyo hilo leo Machi 17,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu zoezi hilo lililoanza leo katika Mkoa wa Dar es Salaam .
Amesema kuwa zoezi hili halihusishwi hata kidogo na kubadilisha kadi zilizokwisha kutolewa na iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, mwaka 2015 na mwaka 2020, kwa mantiki hiyo kadi zile ni halali.
“Kuna taarifa zingine zinazotembea mtandaoni zikipotosha kutokujitokeza kujiandikisha au kuboresha taarifa zao katika daftari la kudumu la mpigakura, kwa hulka za kisiasa au vinginevyo, naomba nitoe rai kwa wananchi wa Dar es Salaam kwamba ni muhimu ukawa na kadi hii ili uweze kupiga kura muda utakapofika.
Na ikibidi kutolalamika, wala kuilalamikia serikali au kutomlalamikia mtu yeyote kwa mwananchi wenye miaka 18 na zaidi mwenye sifa ya kuchagua au kuchaguliwa ni muda muafaka wa kuweza kutii haya masharti haya yote ambayo yametolewa na Tume Huru ya Uchaguzi ili waweze kuwa na sifa hizo zote.”
Aidha amesema kuwa ni vyema wananchi wenye sifa wakatumia siku hizo saba kwakuwa zoezi hilo ni muhimu kwa mustakabali wao na nchi kwa ujumla na kupuuza upotoshaji huo.
“Natoa rai kwa wananchi watumie fursa hii hasa wenye sifa ya kuchagua au kuchaguliwa, nina shauku kuona kila mwana Dar es Salaam anakua mpiga kura, mgombea kwa sifa tajwa ili mkoa uwe kwenye demokrasia sahihi.”amesisitiza RC Chalamila
Hata hivyo amesema kuwa zoezi hilo litaambatana na kuandikisha wapigakura waliotimiza miaka 18 au zaidi au watakaotimiza umri huo tarehe ya uchaguzi, kutoa kadi kwa wananchi ambao kadi zao zimepotea au kuharibika.