14, 15 Machi, 2025,
Kanda ya Ziwa – Serengeti Breweries Limited (SBL) yaimarisha juhudi za maendeleo ya jamii kwa kuzindua mafunzo maalum kwa wanawake na vijana wanaojihusisha na biashara ya usambazaji wa vinywaji katika Kanda ya Ziwa, kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali, Bridge for Change (BFC).
Mpango huu, ambao ni sehemu ya program ya Learning for Life Training ya SBL, unalenga kuwawezesha washiriki kwa kuwapatia ujuzi wa msingi wa biashara na ujasiriamali, ili kuwapa nafasi ya kufanikiwa kwa njia endelevu katika sekta ya usambazaji wa vinywaji.
Wajasiriamali wa awali 50 walichaguliwa kutoka sehemu mbalimbali za Kanda ya Ziwa walipitia mafunzo maalumu yaliyojikita katika maeneo muhimu kama ujuzi wa biashara, elimu ya fedha, usimamizi wa mikopo na hatarishi za kifedha, usimamizi wa bidhaa (inventory management), pamoja na uongozi. Mafunzo haya yalilenga si tu kuboresha ujuzi wa vitendo wa washiriki, bali pia kuwasaidia kukuza biashara zao kwa kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi bora ya kifedha, kuimarisha uendelevu wa biashara, na kuwawezesha kuongeza mauzo kama washirika muhimu katika mfumo wa usambazaji wa SBL.
Akizungumzia umuhimu wa programu hii, Gordon Katundu, Meneja wa Mauzo wa Kanda – Mwanza, kutoka SBL, alisisitiza dhamira ya kampuni katika kuchochea maendeleo jumuishi ya kiuchumi:
“Katika SBL, tunaamini maendeleo ya kweli yanapimwa kwa fursa tunazozalisha kwa jamii zetu. Kupitia program ya Training for Life, tunawekeza moja kwa moja kwa wateja wetu, hususani wanawake na vijana, kwa kuwapatia ujuzi muhimu wa kukuza biashara zao kwa njia endelevu. Hili ni jukumu la moja kwa moja katika afya ya kiuchumi ya jamii, tukiwasaidia washiriki kuimarisha biashara zao na kuleta athari chanya za muda mrefu.”
Kwa upande wake, Ocheck Msuva, Mkurugenzi Mtendaji wa BFC, alieleza manufaa halisi ya mpango huu:
“Tunajivunia kushirikiana na SBL katika kuwezesha mafunzo haya yenye mchango kubwa, ambayo yanakabiliana na changamoto halisi zinazowakumba wajasiriamali. Maarifa yatakayopatikana katika mafunzo haya ni kama usimamizi wa biashara, usimamizi wa mikopo, usimamizi wa kifedha, masoko, na mbinu bora za uendeshaji biashara zitawawezesha washiriki kuwa na ustahimilivu zaidi, kuongeza tija, na kushindana vyema katika sekta ya usambazaji.”
Kupitia mipango ya kimkakati na ushirikiano wa kimaendeleo, SBL inaendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara kwa kuwawezesha wanawake na vijana wengi zaidi kujenga biashara endelevu za usambazaji katika jamii zao. Mpango huu unaonesha kwa dhati jinsi SBL inavyojizatiti kuleta mabadiliko ya muda mrefu ya kijamii na kiuchumi huku ikiimarisha mfumo wa ujasiriamali nchini Tanzania.
Mmoja wa wanufaika, Flora Kimathi, alishiriki uzoefu wake: “Kabla ya mafunzo haya, nilikuwa na uelewa mdogo kuhusu mienendo ya soko na usimamizi wa fedha. Sasa, nimepata mikakati ya muda mrefu itakayonisaidia kuendesha biashara yangu kwa ufanisi zaidi.”
Pia aliwahimiza wajasiriamali vijana kuchangamkia fursa kama hizi: “Nawahimiza vijana wenzangu kutumia mafunzo kama haya, kwani yanatoa maarifa muhimu yanayoweza kubadilisha biashara zao.”