Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa huduma ya maji katika kukuza uchumi na maendeleo ya jamii ya Watanzania.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Mhandisi Zena Said amesema akifungua Mkutano wa Mapitio ya Programu ya Sekta ya Maji jijini Dar es salaam.
Mhandisi Zena akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi katika tukio hilo la Wiki ya Maji amesema fedha inayotolewa na Serikali katika Sekta ya Maji imewezesha huduma ya uhakika wa majisafi kuwafikia wananchi mijini na vijijini.
Ameongeza, Serikali imepania kufanikisha maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kwa jamii, ikiwamo lengo namba sita kuhusu huduma ya majisafi.
Mhandisi Zena amesema Serikali inawashirikisha wadau mbalimbali ili kuongeza nguvu katika masuala mbalimbali ikiwamo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ili kuwa na usalama wa huduma ya maji katika jamii.
Amewataka washiriki wa mkutano huo kutoa maoni kuhusu muendelezo wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ambayo inatarajiwa kukoma mwaka 2026.
Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema Wiki ya Maji ni muendelezo wa kutoa majibu kuhusu changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Maji Duniani.
Amesema Serikali imejipanga kufikisha huduma ya maji kwa asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini na imeweka kipaumbele katika ushirikishwaji wa wadau mbalimbali ili huduma ya maji iwe endelevu.