Mkurugenzi Mtendaji, Ol-aiguenani Meshack Ndaskoi akizungumza kuhusiana na makumbusho hiyo iliyopo jijini Arusha .

Wanafunzi kutoka shule mbalimbali mkoani Arusha walipotembelea makumbusho hiyo jijini Arusha
Happy Lazaro, Arusha.
Wananchi, watafiti pamoja na wanafunzi kutoka ndani na nje ya Jiji la Arusha wameshauriwa kutembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Chifu Ndaskoi iliyopo Moshono, Jijini Arusha kwa lengo la kujionea na kujifunza kuhusu historia ya Jiji la Arusha kabla ya ujio wa wakoloni wakati wa ukoloni na baada ya Uhuru.
Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake kuhusu makumbusho hiyo, Mkurugenzi Mtendaji, Ol-aiguenani Meshack Ndaskoi amesema kuwa makumbusho hii ni taasisi pekee iliyojikita katika kuonesha historia ya Jiji la Arusha, utamaduni na mila za jamii ya Wamaasai ambapo pamoja na maonesho hayo ipo pia bustani ya mimea ambayo ni sehemu ya Makumbusho hiyo.
Amesema kuwa lengo kuu la makumbusho hiyo ni kutoa huduma kwa umma ikiwemo kujifunza, kuelimisha umma, kuweka kumbukumbu, kuhifadhi na kuonesha historia na utamaduni wa Wamaasai, kutafiti na kutangaza utalii.
Amefafanua kuwa, malengo maalumu ni kuongeza uelewa wa wadau kuhusu dhamira na majukumu ya Makumbusho na mchango mkubwa wa Chifu Ndaskoi katika historia ya nchi ya Tanzania.
Aidha ni pamoja na kuelimisha makundi yote katika jamii kushiriki kikamili katika kuhifadhi, kutunza na kukuza urithi wao wa kihistoria na kitamaduni pamoja na kutangaza na kukuza utalii wa ndani na nje na pia kuonesha mila na utamaduni wa jamii ya Wamaasai kupitia vifaa na vyombo halisi kutoka katika jamii hii.
Ameongeza kuwa, lengo lingine ni kujenga mtandao wa ushirikiano kati ya Makumbusho na taasisi za elimu, watafiti, mashirika na taasisi mbalimbali za umma na binafsi, ndani na nje ya nchi.
“Historia ya Arusha inaonesha mtiririko wa baadhi ya matukio yaliyotokea katika nchi II-arusa (Arusha ya sasa) na Meru katika nyakati tofauti kuanzia mwishoni mwa karne ya 16 mpaka sasa na hii inaangazia michango na historia ya Chifu Mkuu Ndaskoi pamoja na mashujaa wengine katika nyanja za ulinzi na usalama, huduma za jamii, elimu, dini, mazingira na uasisi wa Jiji la sasa la Arusha.”
Ameongeza kuwa, chimbuko la makumbusho hiyo ni dukuduku alilokuwa nalo toka akiwa kijana mdogo, pamoja na simulizi za wazee wa Kimaasai kuhusu matukio mbalimbali, historia ya Chifu Mkuu Ndaskoi na mashujaa wengine. Hii ili mhamasisha kufanya utafiti wa kina kuhusu Chifu Ndaskoi na Jiji la Arusha ambao aliufanya kwa takribani miaka 10.
Utafiti huo ulibainisha kuwepo utajiri mkubwa wa kihitoria na kiutamaduni katika Jiji la Arusha pamoja na michango muhimu ya Chifu Mkuu Ndaskoi katika nyanja mbalimbali ikiwamo uongozi, uzalendo, na ushujaa wa kiwango cha juu.
Kwa bahati mbaya historia hii haifahamiki vizuri na watu walio wengi. Aidha wadau walipendekeza kuanzishwa kwa makumbusho ambayo itahusika katika kutafiti zaidi, kuhifadhi na kuonesha kwa umma michango hiyo pamoja na viongozi na Mashujaa wengine wa wakati wake kabla haijapotea kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Amesema kuwa, kupitia makumbusho hiyo utaweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo kuangalia ngoma za jadi za Wamaasai, chakula cha asili cha Wamaasai, kuangalia mlima Meru na vilima vingine jirani, ziara katika vijiji vya Wamaasai.
“Makumbusho hii ni rafiki kwa watu wote na ni ya pekee katika jiji la Arusha kuhifadhi na kuenzi urithi wa kihistoria, kitamaduni, kishujaa ,sanjari na utunzaji na uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema kuwa, huduma hiyo inatoa mchango katika elimu, utafiti, mafunzo na kukuza utalii, na inasaidia kuweka katika muktadha historia ya Chifu Ndaskoi na michango aliyoitoa katika jamii ambayo itakumbukwa daima .
Aidha ameongeza kuwa kwa kutembelea Makumbusho hiyo utapata fursa ya kujionea jinsi mambo yalivyofanyika zamani, hivyo kupata maarifa na ujuzi mpya utakaosaidia kutoa msukumo kwenye ubunifu na uvumbuzi katika Sanaa, teknolojia na tasnia nyingine.
Vilevile amesema kuwa, katika eneo la Makumbusho hiyo pia utapata fursa ya kujionea bustani ya mimea inayohifadhi zaidi ya mimea 250, ambapo bustani yake inatumika kama dawa kwa binadamu na mifugo na inajumuisha miti mitakatifu kwa jamii ya Wamaasai ambapo pia kuna aina kadhaa ya mimea ambayo ipo hatarini kutoweka.
Amesema kuwa, bustani hiyo ni kivutio kwa makundi ya ndege wa aina mbalimbali na ni mwanachama wa taasisi ya kimataifa ya uhifadhi wa bustani za mimea inayojulikana kwa jina la Botanical Garden Conservation International (BGCI) yenye Makao Makuu yake huko Uingereza ikiwa na usajili namba BGCI No. 5442.
Ol-aiguenani Ndaskoi ameiomba Serikali na wadau wengine kusaidia Makumbusho hii ili kuhakikisha kuwa inakuwa endelevu na kuweza kutoa huduma bora zaidi kwa umma na watalii ambapo amesema kuna changamoto ya uhaba wa vitendea kazi mbalimbali vya kiuhifadhi pamoja na miundombinu ya barabara ya kufika eneo hilo kwani sio rafiki ikizingatiwa kwamba watu kutoka maeneo mbalimbali hutembelea kituo hiki.
Amemaliza kwa kuwaalika wakazi wa Arusha, Watanzania kwa ujumla na wageni kutoka nje ya nchi kuitembelea makumbusho hiyo ambayo hutoa huduma zake kila siku kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 11.30 jioni.