Na Silivia Amandius
Kagera
Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera, limependekeza rasmi kubadilishwa kwa jina la Jimbo la Nkenge na kuitwa Jimbo la Missenyi.
Mapendekezo hayo yameungwa mkono na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjat Fatma Mwasa, katika kikao maalum kilichofanyika Machi 17, 2025, katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Katika kikao hicho cha dharura, wajumbe wa RCC walikubaliana na hoja ya Madiwani wa Missenyi, wakibainisha kuwa jina la sasa la Jimbo la Nkenge halihusiani moja kwa moja na Wilaya ya Missenyi, hali inayosababisha changamoto za kiutendaji na mawasiliano kati ya Serikali, chama, na wadau wengine.
Aidha, ilielezwa kuwa jina la “Nkenge” linatambulika zaidi katika muktadha wa Tume Huru ya Uchaguzi na Bunge pekee, jambo linalosababisha mkanganyiko kwa mihimili mingine ya dola kama Serikali na Mahakama, ambapo jina hilo halitumiki katika nyaraka rasmi.
Madiwani walieleza kuwa “Nkenge” ni jina la mto maarufu wilayani Missenyi, unaotenganisha tarafa za Missenyi na Kiziba. Hata hivyo, licha ya umuhimu wake wa kihistoria, wajumbe waliona ni vyema jina la Jimbo lionyeshe uhalisia wa kijiografia na utawala kwa kuitwa Jimbo la Missenyi.
Mabadiliko haya yanatarajiwa kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa hatua zaidi za kisheria na kiutendaji, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha utendaji wa Serikali na uwakilishi wa wananchi.