Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, akizungumza wakati alipokukutana na kufanya mazunguzo na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng ambaye alifika Wizarani hapo kujitambulisha, jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng, akizungumza wakati alipokutana na kufanya mazunguzo na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, akiongoza kikao kati yake na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng, ambaye alifika Wizarani hapo kujitambulisha, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, akiagana na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng ambaye alifika Wizarani hapo kujitambulisha, jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng, wakiongoza ujumbe wa Tanzania na IFAD baada ya kikao ambacho Mkurugenzi huyo alikwenda kujitambulisha, jijini Dodoma. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha – Dodoma)
………..
Na Farida Ramadhani, WF – Dodoma
Tanzania inatarajia kupokea takribani dola milioni 74 kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa ajili ya mazao na program ya kutoa suluhisho la kifedha kwa wakulima wadogo na miradi ya maendeleo vijijini ambayo inaendelea kufanyiwa kazi.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, baada ya kukutana na kufanya mazunguzo na Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng ambaye alifika Wizarani hapo kujitambulisha.
Bi. Amina alisema fedha hizo zitatolewa katika mzunguko wa 13 wa Mfuko huo huku akibainisha kuwa Serikali imekuwa ikishirikiana na IFAD katika kutekeleza progam mbalimbali ikiwemo mazao, kilimo na uvuvi.
“Pamoja na kujitambulisha wamekuja kutueleza malengo yao katika maeneo makuu matatu, ambayo ni uwezeshaji wa wanawake, vijana na lishe”, aliongeza Bi.Amina.
Aidha, aliushukuru Mfuko wa IFAD kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kilimo na uvuvi nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi Mpya wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bw. Sakphouseth Meng, alisema Mfuko huo utaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali hususani katika kilimo na mazao.
Alisema IFAD kupitia miradi yake mbalimbali inayotekelezwa nchini inalenga kuinufaisha jamii hasa katika sekta ya uvuvi, miundombinu, mazao na kilimo.
“Tunapozungumzia watu, tunafanya kazi kwa ajili ya watu na tunajitahidi kuhakikisha kuwa watu wanakuwa kipaumbele chetu. Hili ndilo lengo letu kuu katika uwekezaji kwenye sekta ya uvuvi, miundombinu, mazao na kilimo. Lengo letu la mwisho daima ni kuhakikisha kuwa watu wanapiga hatua katika maisha yao na kuwaondoa kutoka kwenye umaskini”, alisistiza Bw. Meng.
Bw. Meng alisema katika programu zao, wanahakikisha kuwa wanawake wanakuwa na uwezo wa kiuchumi na wanashiriki kikamilifu katika maamuzi kwa kuzingatia mabadiliko ya kijinsia na kuwawezesha wanawake.
Aliongeza kuwa katika program hizo kuna fursa kubwa kwa vijana kushiriki katika biashara ndogo ndogo na ujasiriamali kwa kuanzisha miradi inayowahusisha, ikiwa ni pamoja na kituo cha usindikaji wa maziwa.
Alisema pia wanazingatia upatikanaji wa chakula chenye lishe bora kwa jamii lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa watu wanazalisha chakula lakini pia wanakula vyakula vyenye virutubishi vya kutosha.
Bw. Meng aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufanikisha malengo hayo kwa maendeleo ya Tanzania.