NA BALTAZAR MASHAKA
MFUKO wa Bodi ya Barabara (RBF) umeanika mafanikio yake katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa RBF,Mhandisi Rashid Kalimbaga,ameeleza mafanikio ya mfuko huo leo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa, miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia,serikali imekuwa ikitenga wastani wa sh.bilioni 900 kila mwaka,kugharamia matengenezo ya barabara nchini.
Amesema kuwa fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa wastani wa miradi 700 ya matengenezo ya barabara za kitaifa na miradi 900 ya barabara za wilaya kila mwaka,ambapo miundombinu hiyo thamani yake inakadiriwa kufikia sh.trilioni 39.5,sawa na asilimia 23 ya pato la Taifa..
Kaimu Mtendaji mkuu huyo wa RBF amesema, kwa miaka minne ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita umeonesha juhudi kubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara,pamoja na kuimarisha Mfuko wa Barabara na Bodi yake,kuboresha mtandao wa barabara na hayo ni baadhi ya mafanikio makubwa kupatikana kutokana na usimamizi mzuri na hatua za serikali.
“Serikali kwa kutambua thamani na umuhimu wa barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi,imekuwa ikiimarisha uwezo wa kifedha na kitaasisi kuhakikisha barabara zinakuwa za kisasa ikilenga kuziwezesha kutumika kwa muda mrefu uliopangwa,”amesema.
Aidha,barabara bora zinazohudumia maeneo ya vijijini zimesaidia wananchi kufikia huduma muhimu kama vile elimu,afya,masoko,ajira na fursa nyingine za kiuchumi za kujipatia kipato.
“Miundombinu ya barabara imetumika kama kichocheo cha maendeleo, huku usafiri wa barabara ukiwa njia kuu ya usafiri wa abiria na mizigo, ukiwa na zaidi ya asilimia 90 na 80 ya matumizi ya abiria na mizigo mtawalia.Hii ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya viwanda na uzalishaji wa ajira, hasa katika maeneo ya vijijini,”amesema Mhandisi Kalimbanga.
Pia, Serikali ya awamu ya sita,imeonesha utayari mkubwa katika kukabiliana na changamoto zakukatika kwa mawasiliano kutokana na maafa ya asili kama vile mafuriko,mfano kazi za dharura zilizofanyika Hanang (Manyara) na kurejesha mawasiliano kati ya Dar es Salaam na Mtwara,Aprili 2024, hayo ni mafanikio ya kuhakikisha wananchi wanaendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi bila vikwazo vya miundombinu.
Mhandisi Kalimbanga ameeleza kuwa Mfuko wa Barabara ulianzishwa mwaka 2000 kama juhudi za serikali za kuhakikisha fedha zinapatikana za matengenezo ya barabara, huku tozo ya mafuta inayochangia asilimia 96 ya mapato yote ikiwa chanzo kikuu cha mapato ya Mfuko wa Barabara.
“Kuanzishwa kwa Mfuko wa Barabara kumewezesha upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo ya barabara,hivyo kuimarisha ubora wa miundombinu hiyo ya barabara za kitaifa na wilaya.Serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kuboresha ubora wa barabara nchini,”amesema na kuongeza;
“Barabara za kitaifa zenye hali nzuri zimeongezeka kutoka asilimia 13 mwaka 2000 hadi asilimia 90 leo, huku barabara za wilaya zikiongezeka kutoka asilimia 10 hadi asilimia 60 katika kipindi hicho.Hii inadhihirisha mafanikio makubwa katika kuboresha mtandao wa barabara nchini,jambo ambalo limechangia kuimarisha uchumi na huduma za kijamii.”
Pia,Rais Samia ameimarisha taasisi za usimamizi wa barabara ambazo ni TANROADS, TARURA na Bodi ya Mfuko wa Barabara,kwa kuongeza vitendea kazi na wataalam katika taasisi hizo ambapo serikali imefanikiwa kuhakikisha barabara zinazozalishwa na zinazotumika zinahimili changamoto mbalimbali na zinaendelea kuwa na ubora wa kudumu.
Kaimu Mtendaji mkuu huyo wa RBF amesema imeendelea kufanya kazi kwa juhudi na umahiri mkubwa ili kufikia malengo ya serikali ya awamu ya sita,ambapo ufanisi wa Bodi katika kusimamia fedha na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za matengenezo ya barabara,umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha miundombinu ya barabara nchini.
“Mafanikio ya Mfuko wa Bodi ya Barabara katika miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni ya kupigiwa mfano.Serikali imefanikiwa kuboresha miundombinu ya barabara,hali ya maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi,”alisema Mhandis Kalimbanga.
Pia,kuimarisha uwezo wa kifedha na kitaasisi, serikali imeweza kuhakikisha kuwa barabara nchini zinabaki kuwa za kisasa na zinazotumika kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kalimbanga,mafanikio ya Mfuko wa Bodi ya Barabara katika miaka minne ya uongozi wa Rais Dk.Samia, ni ya kupigiwa mfano ambapo serikali imefanikiwa kuboresha miundombinu ya barabara,hali ya maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
“Tunachukua fursa hii kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ya barabara na hivyo kuiwezesha kutoa mchango unaotarajiwa kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi,”amesema.
Pia, serikali kwa kuimarisha uwezo wa kifedha na kitaasisi,imeweza kuhakikisha kuwa barabara nchini ambazo ni uti wa mgongo wa uchumi na maendeleo ya kijamii zinabaki kuwa za kisasa na kutumika kwa muda mrefu, huku mtandao wa barabara nchini ukiwa na jumla ya kilometa 181,602.2.
Kaimu Mtendaji mkuu huyo wa RBF alisema kati ya kilometa hizo, barabara za za kitaifa ni kilometa 37,225.7 zinazosimamiwa na TANROADS, wilaya kilometa 144,376.5 zikisimamiwa na TARURA.
Hivyo,katika kipindi cha miaka minne cha uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan,Serikali imefanya juhudi kubwa za kuboresha miundombinu ya barabara, kupitia Mfuko wa Bodi ya Barabara (RBF) kutokana na umuhimu wa barabara katika maendeleo ya nchi,kijamii na kiuchumi.