Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele leo Machi 18, 2025 ametembelea baadhi ya vituo vya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Mkoani Dar es Salaam na kushuhudia mwenendo wa zoezi hilo katiuka siku ya kwanza. (Picha na INEC).
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji Rufaa Jacobs Mwambegele akimkabidhi kadi mpya ya Mpiga Kura Ndg. Abubakari Majuto mkazi wa Mzambarauni Kata ya Gongola Mboto Dar es Salaam ambaye ni mlemavu wa viungo alijitokeza kujiandikisha katika kituo cha Shule ya Msingi Mzambarauni leo Machi 18, 2025. (Picha na INEC).
Wananchi wa Kata ya Kongola Mboto jijini Dar es Salaam wakiwa wamejitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboiresha taarifa zao katika kituo cha Shule ya Msingi Mzambarauni Jijini Dar es Salaam. (Picha na INEC).
Na. Mwandishi Wetu
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imesema itaongeza mashine za BVR na watendaji katika vituo ambavyo vimebainika kuwa na watu wengi ili kufanikisha uandikishaji na uborteshaji wa taarifa katika Daftari la Kudumu lka Wapiga Kura mkoani Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele ameyasema hayo leo Machi 18, 2025 katika siku ya pili ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wakati akikagua vituo Mkoani Dar es Salaam.
“Leo katika siku ya pili ya zoezi nimetembelea vituo vya uboreshaji na waliojitokeza wamekua wengi mmno kiasi kwamba vifaa vinaonekana ni vichache, nimeagiza vifaa kwamba viongezwe na vituo viongezwe ili kuweza kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema Mhe. Jaji wa Rufani Mwambegele.
Jaji Mwambegele akiwa katika Kituo cha Lukooni Chanika Jijini Dar es Salaam alishuhudia uwepo wa wananchi wengi waliojitokeza kwaajili ya kuboresha taarifa zao na kujiandikisha na kutoa maagizo ya kuongezwa kwa mashine za BVR katika kituo hicho.
“Hapa Lukooni eneo la Chanika katika Wilaya ya Ilala kulikua na kituo kimoja katika siku ya kwanza, lakini baada ya kubaini kwamba watu wanakua ni wengi na wanatumia muda mrefu nikaagiza vifaa viongezwe na leo nimepita bado nimeona BVR mbili hazitoshi kwahiyo nimeagiza ziongezwe ili kuweza kukabiliana na changamoto hii,” aliongeza Jaji Mwambegele.
Aidha, Jaji Mwambegele amepongeza wananchi wote waliojitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika siku za mwanzo za zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu kwani kufanya hivyo kunawezesha wao kukamilisha zoezi hilo ndani ya siku saba kama ilivyopangwa.
Nae afisa Mwandikishaji wa Jiji la Dar es Salaam, Faraja Nakua amesema katika Majimbo matatu yaliyopo katika Halmashauriu ya Jiji la Dar es Salaam yenye majimbo ya Ilala, Ukonga na Segerea zoezi linakwenda vyema na wao wamejipanga kufanikisha zoezi hilo.
“Nizidi kuwahamasisha wananchi wa Majimbo ya Ukonga, Ilala na Segerea Jijini Dar es Salaam kuendelea kujitokeza kwa wingi na sisi tumejipanga kutekeleza zoezi hili kama ambavyo Tume imeagiza na vifaa tulivyotakiwa kuongeza vipo tutavipeleka katika maeneo yote yenye changamoto,” alisema Nakua.
Nae Atness Shayo mkazi wa Ukonga Mzambarauni na Hassan Said Mmanga wa Chanika wamepongeza ujio wa zoezi hilo kwani walipoteza kadi zao za mpiga Kura na sasa wameoata kadi zao mpya zitakazoweawezesha kupiga Kura katika Uchaguzi Mkuu baadae mwaka huu.
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inataraji kuandikisha Wapiga Kura wapya 643,420 mkoani Dar es Salaam ambapo jumla ya vituo 1,757 vinatumika kwenye uboreshaji kwa mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 96 katika vituo 1,661 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Aidha Tume imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wenye sifa za kuandikishwa wanaandikishwa kwani BVR zaidi ya 5,000 na watendaji wa kutosha wapo kwaajili ya utekelezaji wa zoezi hilo.
Tume imeshakamilisha uboreshaji wa Daftari katika Mikoa 29. Kwa mujibu wa ratiba, leo Tume inaanza uboreshaji katika mzunguko wa 13 ambao ni mzunguko wa mwisho wa uboreshaji wa Daftari. Mzunguko huu unahusisha Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Kailima amesema kwa mkoa wa Dar es Salaam Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 643,420 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapiga kura 3,427,917 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Dar es Salaam utakuwa na wapiga kura 4,071,337 idadi ambayo inaweza kuongezeka kwa kuwa inawezekana wapo watanzania ambao walikuwa na sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura wakati wa uboreshaji wa Daftari mwaka 2019/20, lakini kwa sababu moja au nyingine hawakuweza kujiandikisha.
Zoezi la uboreshaji wa Daftari linahusu kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi na watakaotimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, kutoa kadi mpya kwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika na kutoa fursa kwa wapiga kura walioandikishwa kurekebisha taarifa zao yakiwemo majina na taarifa nyingine.
Uboreshaji wa Daftari pia unahusu kutoa fursa kwa wapiga kura waliopo kwenye Daftari na ambao wamehama, waweze kuhamisha taarifa zao kutoka kata au jimbo walipoandikishwa awali na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo kwenye Daftari kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa Tanzania na kifo.