Na Silivia Amandius.
Kagera:
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa Katoliki katika kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia utoaji wa huduma muhimu za kijamii kama afya, elimu na maji.
Ametoa kauli hiyo leo, Machi 19, 2025, aliposhiriki maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Mstaafu Mhashamu Methodius Kilaini, yaliyofanyika katika Kanisa Katoliki, Jimbo la Bukoba, mkoani Kagera.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema Kanisa Katoliki limekuwa mstari wa mbele katika kujenga miundombinu ya kijamii, hususan katika sekta ya afya na elimu, na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za kidini katika kutoa huduma kwa wananchi bila kuvunja misingi ya kikatiba.
“Serikali itaendeleza ushirikiano na makanisa na misikiti katika kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii, huku ikipokea ushauri kutoka kwa viongozi wa dini ili kuimarisha maendeleo ya nchi yetu,” alisema Majaliwa.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali inatambua nafasi ya viongozi wa dini katika jamii, hasa katika kuhamasisha maadili mema kwa vijana kupitia mahubiri na mawaidha yanayotolewa katika nyumba za ibada.
“Nguvu ya imani kupitia mahubiri ni njia mojawapo ya kurudisha maadili ya Kitanzania yenye misingi ya utu, haki na amani, ambayo ni msingi wa taifa letu,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Bi Fatma Mwassa, alisema viongozi wa dini wamekuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya mkoa kwa kutoa ushauri wa kiutendaji, hasa katika sekta za uchumi na huduma za kijamii.
Akimpongeza Askofu Mstaafu Kilaini, Mwassa alieleza kuwa amekuwa msaada mkubwa, hususan katika usimamizi wa huduma za afya akiwa mjumbe wa bodi ya hospitali, akichangia maarifa kutokana na uzoefu wake mkubwa ndani ya kanisa.
“Askofu Kilaini alishiriki kikamilifu katika kuboresha huduma za afya kwa kutumia uzoefu alioupata akiwa mwanzilishi na msimamizi