Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 19, 2025.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 19, 2025, kushoto ni Mhe. Samwel M. Maneno, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali
……………….
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Serikali inaendelea kuchukua hatua za kuboresha utendaji wa mawakili wake kwa kuwaandalia mafunzo maalum yanayolenga kuimarisha uelewa na ufanisi wao katika mikataba ya ndani na ya kimataifa, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, na utungaji wa sheria.
Zaidi ya mawakili 300 wa serikali wanatarajiwa kushiriki katika mafunzo hayo yatakayofanyika jijini Arusha kuanzia Machi 24 hadi 28, 2025, yakihusisha wataalamu wa sheria kutoka ndani na nje ya nchi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza Johari, akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 19, 2025, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo mawakili hao ili kuhakikisha wanakuwa na ujuzi wa kina kuhusu misingi ya mikataba na mazungumzo ya kimkataba.
“Mawakili wa Serikali watajifunza misingi ya mikataba, ujuzi maalum unaohitajika katika mazungumzo ya mikataba, pamoja na miiko inayopaswa kuzingatiwa katika meza ya majadiliano. Hii ni muhimu hasa kwa kuzingatia kuwa Tanzania inaendelea kuvutia wawekezaji wengi zaidi, na hivyo idadi ya mikataba inaongezeka,” amesema Johari.
Ameeleza kuwa mafunzo hayo pia yatazingatia usuluhishi wa migogoro ya kibiashara ili kuhakikisha kuwa migogoro inayotokana na mikataba inashughulikiwa kwa ufanisi na kwa maslahi ya taifa.
“Katika mikataba mingi, kuna uwezekano wa kutokea migogoro. Tunataka kuhakikisha kuwa mawakili wa serikali wanakuwa mahiri katika kushughulikia migogoro hiyo kwa njia za kisheria na usuluhishi,” amesema.
Aidha, amesema mafunzo hayo yataangazia pia utungaji na uandishi wa sheria, ambao ni eneo linalohitaji utaalamu maalum kwa kuzingatia misingi na kanuni za kisheria.
“Tutajadili pia wajibu wa mawakili katika kulinda maslahi na usalama wa taifa. Ni muhimu kwao kuelewa kwamba kazi yao si tu kufanikisha mikataba bali pia kuhakikisha kuwa taifa halihatarishi maslahi yake ya kiuchumi na kijamii kwa kushindwa kusimamia vipengele muhimu vya kisheria,” amesema Johari.
Mafunzo haya yanakuja wakati ambapo Tanzania inaendelea na jitihada za kuboresha mazingira ya uwekezaji, huku dira ya maendeleo ya 2050 ikisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya kisheria na kiutawala.