Na John Bukuku
Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuboresha sekta ya afya na kuhakikisha huduma zinapatikana kwa urahisi.
Katika kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizi, idadi ya bidhaa za afya ashiria zinazotumika kupima hali ya upatikanaji imeongezeka kutoka 290 mwaka wa fedha 2021/22 hadi bidhaa 382 mwaka wa fedha 2023/24. Hali ya upatikanaji wa bidhaa hizo imeongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2021/22 hadi asilimia 67 kufikia Februari 2025, sawa na ongezeko la asilimia 23.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Bw. Tukai Mavere, alisema kuwa bohari hiyo imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika vifaa tiba ili kuboresha huduma za afya nchini. “Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, MSD imefanya ununuzi na usambazaji wa vifaa tiba vinavyohitajika katika vituo vya afya, kuanzia ngazi ya msingi hadi hospitali za kibingwa na ubingwa bobezi,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Mavere, vifaa hivyo vimewezesha kuboresha huduma za uchunguzi wa magonjwa na tiba, ambapo baadhi ya vifaa vilivyonunuliwa ni mashine za usingizi, CT-Scan, MRI 3T, mashine za Ultrasound, na digital X-Ray zenye thamani ya shilingi bilioni 376.6.
MSD pia imeendelea kusimamia upatikanaji wa bidhaa muhimu kwa ajili ya magonjwa maalum kama UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu, na Ukoma kupitia Mradi Msonge. “Utekelezaji wa mradi huu umeimarishwa kutoka asilimia 18 mwaka 2022 hadi asilimia 97 kufikia Desemba 2024, ikiwa ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Global Fund mzunguko wa sita (GC6),” alisema Bw. Mavere.
Aidha, serikali imeongeza usambazaji wa vyandarua kwa ajili ya kupambana na malaria, ambapo mwaka 2021 vilisambazwa vyandarua 7,209,932, huku mwaka 2023 idadi hiyo iliongezeka hadi 9,796,509, sawa na ongezeko la asilimia 36.
Bw. Mavere alieleza kuwa, kutokana na changamoto za kimataifa zinazoathiri ugavi na uzalishaji wa bidhaa, upatikanaji wa bidhaa za afya ulifikia asilimia 79 hadi Juni 2024, lakini ukashuka hadi asilimia 67. Hata hivyo, serikali imechukua hatua ya kununua bidhaa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji na inatarajia kufikia asilimia 90 ifikapo Juni 2025.
Katika sekta ya uchujaji wa damu (dialysis), Bw. Mavere alisema MSD imeendelea kuwekeza ili kupunguza gharama za matibabu ya figo kwa wananchi. “Hadi Februari 2025, mashine za hemodialysis zimeongezeka kutoka 60 mwaka wa fedha 2021/22 hadi 137, huku hospitali zinazotoa huduma hiyo zikiongezeka kutoka 6 hadi 15,” alisema. Uwekezaji huu umegharimu shilingi bilioni 7.7.
Miongoni mwa hospitali zinazotoa huduma za dialysis ni Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Amana, Mwananyamala, Temeke, Morogoro, Katavi, Tumbi, Chato, Sekou Toure, na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Serikali inatarajia kupunguza gharama za huduma hiyo kutoka shilingi 200,000-230,000 kwa kila ‘session’ hadi chini ya shilingi 100,000.
Katika juhudi za kuboresha afya ya kinywa na meno, Bw. Mavere alieleza kuwa MSD imeongeza usambazaji wa bidhaa za afya hiyo, ambapo mwaka wa fedha 2024/25 imesambaza bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 9.98, ikilinganishwa na shilingi milioni 254.7 mwaka 2021/22. “Kwa kipindi cha miaka minne, jumla ya bidhaa za afya ya kinywa na meno zenye thamani ya shilingi bilioni 21.5 zimesambazwa, huku viti vya huduma za meno vikigharimu shilingi bilioni 13.8 na mashine za kisasa za mionzi ya meno zikiwa na thamani ya shilingi bilioni 4.07,” alisema.
Serikali pia imeendelea kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kusambaza vifaa na bidhaa muhimu kwa vituo vya afya 316 vinavyotoa huduma za dharura za uzazi (CEmONC). Jumla ya bidhaa 414 zenye thamani ya shilingi bilioni 100.2 zimesambazwa katika vituo hivyo.
Kwa mujibu wa Bw. Mavere, MSD imeongeza idadi ya mizunguko ya usambazaji kutoka minne (kila baada ya miezi mitatu) hadi sita (kila baada ya miezi miwili), ambapo hali ya usambazaji kwa wakati imeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2021/22 hadi asilimia 98 mwaka 2024/25.
Kuhusu mapato ya MSD, Bw. Mavere alisema kuwa kutokana na maboresho yanayoendelea, mapato ya Bohari ya Dawa yameongezeka kutoka shilingi bilioni 315.1 mwaka wa fedha 2021/22 hadi shilingi bilioni 553.1 mwaka wa fedha 2023/24, sawa na ongezeko la asilimia 76. “Hadi Februari 2025, MSD imekusanya mapato ya shilingi bilioni 400.2, ambayo ni asilimia 115 ya lengo lake la kusambaza bidhaa za afya zenye thamani ya shilingi bilioni 346.6,” alisema.
Maboresho haya yanaendelea kuimarisha sekta ya afya nchini, huku serikali ikiweka mikakati ya kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wananchi wote kwa gharama nafuu na kwa wakati.