Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Mhe. Onesmo Buswelu hivi karibuni, katika kikao kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya.
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme akichangia wakati wa kikao kilichoongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis na kufanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Mhe. Onesmo Buswelu.
Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Mhe. Onesmo Buswelu akitoa neno la ukaribisho wakati wa kikao kilichoongozwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis (kulia) na kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya.
…….
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema biashara ya kaboni ni nyenzo muhimu katika kukuza uchumi hivyo ni muhimu ikapewa msukumo.
Akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi Mhe. Onesmo Buswelu hivi karibuni, Naibu Waziri Khamis amesema yapo mafanikio yanayopatikana kutokana na biashara hiyo yakiwemo utekelezaji wa miradi kutokana na fedha zinazotokana na biashara ya kaboni.
Mhe. Khamis amesema kuwa biashara ya kaboni ni fursa adhimu inayoingiza fedha ambazo huwezesha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ambayo ni muhimu kwa jamii ikiwemo ya elimu, afya na maji.
Naibu Waziri Khamis aliwapongeza viongozi wa Wilaya ya Tanganyika kwa kusimamia vyema misitu iliyopo katika eneo hilo ambayo mbali na kuwa chanzo cha hifadhi endelevu ya mazingira lakini pia huleta faida hususan katika biashara ya kaboni.
Aliwasihi wanananchi kuendelea kupanda miti na kuitunza ili iendelee kuwa kichocheo cha uchumi kutokana na biashara ya kaboni ambayo tayari Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa kanuni na mwongozo wa usimamizi wake.
Aidha, Mhe. Khamis ambaye katika kikao hicho aliambatana na viongozi na watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, alibainisha kuwa misitu husaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo kila mtu anapaswa kushiriki kikamilifu katika kampeni za upandaji miti.
Alisema pamoja na masuala mbalimbali Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa jamii ili kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa, hali inayochangia uharibifu wa mazingira.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa Urejeshwaji Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) ambao utasaidia jamii ya wilaya hiyo kuachana na shughuli za uharibifu wa mazingira zinazotokana na ukataji wa miti na hivyo kuendelea kutunza misitu iliyopo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme alizipongeza taasisi zilizoanza kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Alisema matumizi ya nishati safi ya kupikia husaidia kuepuka changamoto za kiafya zinazotokana na kuvuta moshi endapo utapikia nishati isiyo safi ikiwemo kuni na mkaa.
Vilevile, Bi. Mndeme alisema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia hupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa na hivyo kusaidia katika kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake Mhe. Buswelu ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji wa miradi katika wilaya hiyo na kusema kuwa inasaidia katika hifadhi ya mazingira.
Alisema kuwa Wilaya ya Tanganyika na Mkoa wa Katavi kwa ujumla inafanya vizuri katika sekta ya hifadhi ya mazingira hususan kupitia misitu iliyopo katika maeneo hayo.
Aliongeza kuwa Mradi wa SLR unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais unasaidia katika kukuza kipato cha wananchi kwani wamewezeshwa kufanya shughuli zisioharibu mazingira.