Na John Walter -Babati
Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Burunge (JUHIBU) imeendelea kubuni mbinu mbalimbali za kuzuia wanyamapori waharibifu kuvamia mashamba na kula mazao ya wakulima.
Katika juhudi hizo, JUHIBU imeanzisha matumizi ya baruti, pilipili na mchanga vilivyowekwa kwenye mipira ya kondomu kama moja ya njia za kuwazuia wanyama hao kuingia kwenye mashamba ya wananchi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuela Kaganda, amekabidhi vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 76 vya kuimarisha ulinzi wa mashamba kwa vijiji 10 vinavyohudumiwa na JUHIBU.
Kwa mujibu wa Katibu wa JUHIBU Benson Mwaise, Vifaa hivyo ni pamoja na vilipuzi na honi, ambavyo vinalenga kusaidia wakulima kuwatisha wanyama waharibifu na hivyo kuwaepusha na hasara ya mazao yao.
Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, hasa katika maeneo yanayopakana na hifadhi za wanyama.
“Tunapenda kuona wakulima wakiendelea kufanya shughuli zao bila hofu ya wanyama waharibifu, huku tukihakikisha kuwa wanyama hawa wanahifadhiwa kwa njia endelevu,” alisema Kaganda.
JUHIBU imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhisho endelevu kwa changamoto hii, kwa kushirikiana na serikali na wananchi kuhakikisha wanyama na binadamu wanaishi kwa amani bila kuathiri ustawi wa pande zote mbili.