TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UANDIKISHAJI WA WAPIGA KURA MKOA WA DAR ES SALAAM
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkoa wa Dar es salaam, pamoja na zoezi hilo kuendelea vizuri kumejitokeza changamoto ya baadhi ya watu kujiandikisha zaidi ya mara moja katika vituo tofauti. Kuhusu suala hili,
napenda kutoa taarifa ifuatayo:
- Baada ya zoezi la uandikishaji kukamilika katika vituo, Tume huchakata
taarifa za watu wote walioandikishwa kupitia mfumo maalum (Automatic Fingerprint Identification System–AFIS), ambao una uwezo wa kuwabaini wapiga kura wote waliojiandikisha zaidi ya mara moja.
- Aidha, Tume hufanya zoezi la kulinganisha sura za watu wote waliopo kwenda Daftari lengo ni kubaini iwapo kuna waliojiandikisha zaidi ya
mara moja.
- Iwapo itabainika mtu amejiandikisha zaidi ya mara moja. Yafuatayo
yatafanyika:
(i) Jina na taarifa za mtu huyo, hufutwa na mfumo katika vituo
vingine na kubakizwa katika kituo cha mwisho alichojiandikisha
katika Daftari. HIVYO, TAARIFA NYINGINE ZOTE ZA AWALI
HUFUTWA.
m
1
(ii) Kwa mujibu wa masharti ya Kifungu cha 114(1) cha Sheria ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na.1 ya Mwaka 2024 kujiandikisha zaida ya mara moja ni kosa la jinai na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua kiasi cha shilingi laki moja (100,000/=) na isiyozidi shilingi laki tatu (300,000/=) au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja, kulipa faini na kifungo gerezani.
(iii) Baada ya uchakataji wa Daftari kwa mfumo wa AFIS watakaobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, orodha yao itakabidhiwa Jeshi la Polisi kwa hatua za kisheria; na
(iv) Mpiga kura atakayejiandikisha zaidi ya mara moja, mbali ya kutenda kosa anaweza kushindwa kupiga kura kwa kuwa atafutwa katika vituo alivyojiandikisha na kuachwa kituo cha mwisho pengine siyo kituo chake sahihi anachopaswa kupiga
kura.
Tunatoa wito kwa wakazi wa Dar es salaam kuendelea kujitokeza katika siku
nne zilizosalia kufikia tarehe 23 Machi, 2025 na tunaendelea kufuatilia zoezi
hilo kwa karibu ili kila mwananchi aliyestahili kuandikishwa au kuboresha taarifa zake anapata haki hiyo.
Imetolewa leo tarehe 20 Machi, 2025 na
Kallima, R.K
rage
MKURUGENZI WA UCHAGUZI
KUJIANDIKISHA KUWA MPIGA KURA NI MSINGI WA UCHAGUZI BORA