Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makori,akisalimiana na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilaya kabla ya kufungua mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa St Kilian Mbinga Mjini.
Baadhi ya Walimu wa shule za Msingi na Sekondari Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakiimba wimbo maalum wa mshikamo wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika katika Ukumbi wa St Kilian Mbinga Mjini.
Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Kisare Makori,akikata keki kuashiria mwaka mpya wa Chama cha Walimu Tanzania,baada ya kufungua Mkutano maalum wa kuchagua viongozi wa Chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ambapo Mwalimu Nicosem Hyera amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti baada ya kupata kura 285 kati ya 287,kushoto aliyeshika kipaza sauti Katibu wa CWT Wilaya ya Mbinga Chacha Maro.
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania(CWT) anayewakilisha Mkoa wa Ruvuma Mwalimu Sabina Lipukila,akilishwa kipande cha keki na Mkuu wa Wilaya ya Mbinda Kisare Makori baada ya kukamilika kwa zoezi la kuchagua viongozi wa Chama hicho Wilaya ya Mbinga,katikati Mwenyekiti wa CWT Mkoani Ruvuma Kalimeje Sandali.
Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,wakimsikiliza Katibu wa Chama hicho Chacha Maro(hayupo Pichani) kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika katika Ukumbi wa St Kilian Mbinga mjini,
…………….
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
SERIKALI ya Wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma,imewataka Walimu wa Wilaya hiyo kujiepusha na masuala ya Siasa wanapokuwa kazini, badala yake wafanye kazi kwa kufuata sheria,kanuni na miongozi inayosimamia sekta ya elimu ili kuepuka athari na migogoro sehemu ya kazi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Kisare Makori,wakati akizungumza na wawakilishi wa walimu wa shule za Msingi na Sekondari kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilaya ya Mbinga uliofanyika katika ukumbi wa St Kiliani Mbinga Mjini.
“Nawaomba sana walimu wangu tuepukane na mambo ya Siasa na migogoro isiyo na tija,tumia kila dakika uliyonayo kujiuliza umefanya nini kwenye taaluma yako ili kuleta manufaa katika maisha yako mwenyewe na sehemu ya kazi”alisema Makori.
Alisema,Serikali inatambua kuwa walimu ni msingi wa maendeleo ya Taifa letu na hakuna Taifa lolote Duniani linaloweza kupiga hatua ya maendeleo bila kuwa na walimu bora na mazingira mazuri ya kufundishia.
Alisema,kwa kutambua umuhimu huo ndiyo maana Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,inafanya juhudi kubwa kuboresha sekta ya elimu na hali ya walimu nchini.
Alisema,Watanzania ni mashahidi wa kazi kubwa inayofanywa na Serikali kuhakikisha walimu wanaboreshewa mazingira mazuri ya kufanyia kazi,kutatua changamoto zao ikiwemo kupandisha madaraja kwa wakati kwa mujibu wa mwongozo wa utumishi wa umma ili kuongeza motisha kazini.
Amewasisitiza kufanya kazi kwa weledi,kushirikiana na Serikali katika sekta ya elimu kwa manufaa ya Taifa letu na kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kuwa na Walimu wenye ujuzi kulingana na mahitaji ya sasa kwa kuwa Serikali inawaamini.
Mkuu wa Wilaya,amewaomba walimu kuwa mabalozi wazuri kwa kuwahamasisha wananchi wajitokeze kwenye uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura na kuwaeleza umuhimu wa kuchagua viongozi bora kwenye Uchaguzi wa Mwezi Oktoba mwaka huu.
Katika hatua nyingine,amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na Halmashauri ya Mji Mbinga,kutumia mapato ya ndani kulipa madeni ya walimu kwani itawezesha kufanya kazi kwa kujituma na kuongeza kiwango cha taaluma kwa watoto mashuleni.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilaya ya Mbinga Chacha Maro,amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kubadili muundo wa Utumishi wa walimu ulioongeza ukomo wa madaraja kulingana na viwango vya elimu na kuongeza madaraja mawili kwa kila kiwango.
“kwa mfano mwalimu wa cheti alikuwa anaishi daraja E ila sasa wanaenda mpaka daraja G ambapo Chama cha Walimu kiliomba na hatimaye Serikali ya imetekeleza”alisema Chacha.
Alieleza kuwa,kwa sasa mioyo yao ina furaha kubwa kutokana na mambo makubwa na mazuri aliyoyafanya Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi kifupi cha utawala wake.
Kwa mujibu wa Chacha,pamoja na mafanikio hayo lakini changamoto kubwa ni suala la kikokotoo kwani wastaafu wanapomaliza utumishi wa umma wanapokea fedha kidogo ambayo haikidhi kujikimu na ameiomba Serikali kuangalia upya suala la kikokoto kwa wastaafu.
Chacha, ametaja changamoto nyingine ni upungufu wa walimu na nyumba za walimu kwani zilizopo ni chache na hazitoshelezi hususani maeneo ya vijijini ambako hata nyumba za kupanga hazipo na kumfanya mwalimu kutafuta makazi mbali na maeneo ya kazi.
Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Mbinga Nicomdem Hyera,amewaomba walimu viongozi kwenda kukusanya matatizo ya walimu na kuyafikisha kwenye ngazi ya wilaya li yaweze kufanyiwa kazi na Serikali.
Afisa elimu wa Mkoa wa Ruvuma Judith Mpenzile alisema,Mkoa huo bado uko nyuma kitaaluma kwa hiyo walimu wana kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha taaluma inaongezeka.