Jeshi la Polisi nchini limeendelea kuwatambua askari Polisi wanaotekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu na kuwapatia sifa na zawadi kutokana na kitendo chao cha kuliletea sifa Jeshi hilo kwa kuonesha uwajibikaji kwenye utekelezaji wa maelekezo na maagizo mbalimbali kutoka kwa viongozi wao.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa Sifa na Zawadi kwa askari Polisi sita (6) waliofanya vizuri zaidi kwa mwaka 2024, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Dkt. Lazaro Benedict Mambosasa amesema, askari hao wameonesha weledi mkubwa katika uwajibikaji wao, ufuatiliaji wa miongozo mbalimbali ambayo imesaidia kuleta mafanikio ndani ya Jeshi la Polisi.
Aidha, DCP Dkt. Lazaro Mambosasa, amewapongeza wadau mbalimbali wanaoendelea kushirikiana na Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es salaam katika maeneo tofauti ikiwemo masuala ya kitaaluma huku akitoa wito kwa askari wa vyeo mbalimbali kuendelea kujituma na Kutenda kwa weledi na uadilifu bila kusimamiwa kwa kuhakikisha wanatafuta ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza ndani ya jamii ikiwemo uhalifu na wahalifu.