Na Mwandishi wetu Dodima
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF),Peter Ilomo amewataka waratibu wa mfuko huo wa halmashauri na mikoa,kuhakikisha walengwa waliohitimu kupokea fedha za Kaya maskini,hawatoki katika vikundi vya ujasiriamali,ili wazidi kujiinua kiuchumi.
Ilomo ameyabainisha hayo Wilayani Kongwa mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa nyumba za walimu pamoja na shule uliotekelezwa na TASAF kwa kushirikiana na wananchi wa Kata ya Chitego iliopo wilayani Kongwa.
Aidha amesema walengwa hao hawapaswi kuondoka katika vikundi hivyo,badala yake wanapaswa kubaki ili kuendelea kutoa elimu kwa walenga wengine wanaoingia katika mpango huo kwa ajili ya kuwaelekeza namna ya kutunza fedha hizo ili waweze kujikwamua kiuchumi.
“Naomba muwape elimu walengwa waliohitimu kupokea fedha za mpango wa TASAF,ya kuwa hawapaswi kutoka badala yake wakae kuwafundisha wanaoanza kupokea fedha za mfuko huo ili wasonge mbele,”alisema Ilomo.
Amesema pia lengo la TASAF, ni kuona walengwa wote wanapiga hatua kimaendeleo kutokana na fedha wanazopewa na mfuko huo kwa ajili ya kujikimu wao na familia zao katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Naye Diwani wa Kata ya Chitego Peter Kalunju amesema TASAF imekuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa eneo hilo,hivyo yeye kama Diwani wataendelea kushirikiana na TASAF ili kuhakikisha wakazi wa eneo hilo wananufaika na mfuko huo.
Kalunju amesema TASAF imekuwa ikisaidia vitu vingi katika kata hiyo,zikiwemo nyumba za walimu pamoja na shule kitendo ambacho kimewasaidia wanafunzi kupata elimu katika eneo la kijiji hicho lakini wanakijiji kutanua wigo wa kufanya biashara ndogo ndogo.
“Tunaishkuru sana serikali kwa kuweka mpango huu wa TASAF unasaidia sana wananchi wasiojiweza kuinuka kiuchumi kupitia fedha wanazozipatiwa na mfuko huo,”alisema Kalunju.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa wilaya ya kongwa,waliokuwa wakikabiliwa na hali duni ya maisha wameishukuru Serikali kwa kubuni mpango huo ambao unaleta matokeo chanya kwa jamii.
Amesema utaratibu wa serikali ya Tanzania kuzisaidia kaya maskini, kupitia mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf kwa njia ya utoaji fedha kwa walengwa katika maeneo mbalimbali Una manufaa makubwa kwa jamii.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Kongwa Fortunatus Mabula,aliwashkuru TASAF kutokana na kutembelea miradi wanayo tekeleza ili kuhakikisha inakuwa salama ikiwemo kusimamiwa.
Mabula amesema lengo lao ni kuona wanufaika wote wanapiga hatua kufanya ujasiriamali mbalimbali ili kuhakikisha wanapiga hatua ikiwemo kuinuka kiuchumi.