Na Mwandishi wetu, Babati
WAKALA wa barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Manyara, imeandaa mapendekezo ya mpango wa bajeti ya shilingi 11,529.313 kwa ajili ya kazi za matengenezo na shilingi 164,554.267 ya kazi za maendeleo kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara, Dutu Masele ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha ushauri kamati ya mkoa huo (RCC) kilichofanyika hivi karibuni mjini Babati.
Masele amesema baadhi ya matengenezo ni lami ya kawaida, lami ya muda maalum, madaraja madogo na makubwa, barabara za changarawe na maeneo korofi.
Amesema kazi za matengenezo iliyopangwa ni kuendelea kuweka tabaka la lami sehemu zilizochakaa katika barabara kuu za Babati-Singida na Babati-Arusha.
Ametaja mengine ni kuendelea kuzifanyia matengenezo barabara kwa kuchonga na kuweka changarawe sehemu korofi na matengenezo madogo ya madaraja.
“Ujenzi wa kiwango cha zege mlima Magara katika barabara ya mbuyu wa mjerumani-Mbulu, kujenga daraja Ngolei barabara kuu ya Bereko-Babati-Minjingu,daraja la Dabil na kupendezesha miji na kuweka taa za barabarani maeneo ya mijini,” amesema.
Meneja amesema kutakuwa na ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya Singe-Sukuro sehemu ya kibanda cha maziwa hadi soko la mazao Gallapo kwa ajili ya kuborsha usafiri na usafirishaji wa mazao.
Amesema kutakuwa na kuchepusha ujenzi wa kilomita moja ya barabara ya Orkesumet mjini – Gunge na ujenzi wa kiwango cha lami kilomita moja ya barabara kwenye eneo Dongobesh.
Masele amesema kutakuwa na ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya kilomita moja kuanzia Sawe (Kwa Nadee) kuelekea Daghailoy na kuchonga na kuweka changarawe katika barabara mbalimbali za mkoa.
“Kulipa fidia ya mali zitakazoathirika na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika barabara ya Singe-Kimotorok-Ngopito, Mbuyu wa mjerumani-Mbulu-Mogitu-Haydom na Dareda-Dongobesh,” amesema.
Amesema watajenga barabara ya kiwango cha lami ya Dareda Centre – Dareda Mission kilomita saba na kuinua tuta la barabara kati ya Maweni na Magara.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amepongeza utendaji kazi wa TANROADS katika kutunza na kuhudumia barabara za mkoa huo.