Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemtangaza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Yakub Janabi kuwa Mgombea wa Nafasi ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika.
Akibainisha sifa na uwezo binafsi wa mgombea huyo katika mkutano na waandishi wa habari, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama (Mb.) amesema kuwa Prof. Janab ni mgombea sahihi mwenye uwezo wa kazi na kufanya mageuzi pamoja na maboresho katika sekta ya afya.
Aidha, ameeleza kuwa Prof. Janabi amehudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwa ni pamoja na kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo ameshiriki katika kuleta mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma bora za afya na kuimarisha mifumo ya rufaa kutoka vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi mpaka Taifa.
Vilevile amesema kuwa, akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza na mwanzilishi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof. Janabi aliongoza mageuzi makubwa katika huduma za matibabu ya moyo nchini Tanzania na barani Afrika. Mageuzi haya yameleta mafanikio makubwa, ikiwemo kupungua kwa asilimia 95 ya rufaa za wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi, na kuimarisha utoaji wa huduma za matibabu ya moyo katika kanda ya Afrika.
“Tanzania, kupitia mgombea wetu, Prof. Janabi, ina imani kubwa ya kushinda katika uchaguzi huu kutokana na maono yake ya kuunganisha nguvu za pamoja kwa ajili ya kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya afya barani Afrika. Uzoefu wake wa muda mrefu katika sekta ya afya, uongozi wake madhubuti, na mchango wake mkubwa katika maboresho ya huduma za matibabu ndani na nje ya nchi, ni vigezo vinavyomfanya kuwa kiongozi bora wa kuboresha afya ya wananchi wa Afrika,” alifafanua Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama pia, ametoa wito kwa Watanzania na wadau wa sekta ya afya kushirikiana katika kumnadi Prof. Janabi, akisisitiza kuwa ushindi wake utasaidia kuimarisha mifumo ya afya Afrika na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wote wa bara hili.