Na John Walter -Babati
Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) mjini Babati umefanya matembezi maalum katika viunga vya mji huo, wakimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na mingine katika kila kata, wilaya, na mkoa ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.
Matembezi hayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM mjini Babati, Magdalena Uronu, ambaye aliwataka vijana kuendelea kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa amefanya mambo muhimu katika Jimbo hilo kwenye kila sekta.
Amesema kuwa wanapokaribia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ni muhimu vijana kuonyesha mshikamano na kuendeleza uungwaji mkono kwa serikali inayoendelea kutekeleza maendeleo kwa vitendo.
Katika matembezi hayo, vijana walibeba mabango yenye ujumbe wa kumpongeza Rais Samia, huku moja ya mabango yakisomeka:
“Mama, Vijana wa mjini Babati hatuna deni na wewe, sisi ndio unatudai, tutakulipa ifikapo Oktoba 2025.”
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Babati Mjini, Elizabeth Malley, alisema kuwa Rais Samia ameitekeleza Ilani ya CCM kwa ufanisi kama ilivyoelekezwa kwa kipindi cha 2020-2025, na kuwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na chama hicho.
Naye Katibu wa Itikadi, Mafunzo, na Uenezi wa Mkoa wa Manyara, John Nzwalile, amesema kuwa kwa kazi kubwa iliyofanywa na CCM chini ya Rais Samia, upinzani hautakuwa na nafasi katika uchaguzi ujao.
Amesisitiza kuwa maendeleo yanayoonekana ni ishara kuwa wananchi wataendelea kuiamini CCM.
Matembezi haya yamebeba ujumbe wa mshikamano na uungwaji mkono kwa Rais Samia huku yakihamasisha kauli mbiu mpya ya Chama cha Mapinduzi kwa kipindi cha 2025-2030: “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.”