Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi kwa Wizara ya Maji kutokana na kasi ya utendaji wake katika sekta ya maji nchini na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji safi na salama.
Rais Dkt. Samia amesema hayo leo katika kilele cha Wiki ya Maji iliyokwenda sambamba na Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002 Toleo la 2025 katika Ukumbi wa Mlimani City.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Shirika B. Nyanga imesema Katika hotuba yake Rais Dkt. Samia amesema kutokana na umuhimu wa sekta ya maji kwa uhai, ustawi, ajira na utulivu wa nchi, Serikali imeweka mkazo katika kusimamia miradi ya maji hali iliyoimarisha huduma za maji nchini.
Kuhusu hali ya upatikanaji wa maji, Rais Dkt. Samia ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya maji nchini, ambapo upatikanaji maji vijijini hadi sasa ni asilimia 83% ikiwa imebaki asilimia 2% kutimiza ahadi iliyotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025. Vilevile, kwa mjini upatikanaji wa maji ni asilimia 95%.
Hata hivyo, amesema pamoja na mafanikio yaliyoshuhudiwa nchini, ni lazima baadhi ya mambo yabadilike ili wananchi waendelee kunufaika na upatikanaji endelevu wa maji safi na salama.
Rais Dkt. Samia ameongeza kuwa katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maji iliyoboreshwa, Serikali inapaswa kujihadhari dhidi ya matishio kwa usalama wa chakula, athari za mabadiliko ya Tabianchi na mabadiliko ya siasa za dunia.
Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa ili kuwa na upatikanaji maji endelevu lazima wananchi washirikiane na Serikali kutunza na kulinda vyanzo vyote vya maji. Pia amewataka Watanzania kulinda miundombinu ya maji iliyojengwa kwa gharama kubwa na ili kuepusha na madhara kwa afya ya watumiaji wa maji ikiwa mabomba makubwa yatapasuka.
Kwa upekee Rais Dkt. Samia ameelekeza kuimarishwa kwa miradi ya kuvuna maji ya mvua ambapo alikumbusha kuwa hilo ni agizo la siku nyingi.
“Ninakumbuka kwa mara ya kwanza kuiona Dodoma nilikwenda kwa ajili ya mazungumzo ya uvunaji maji ya mvua. Hakika kila tone la maji lina thamani, iwe maji ya mvua au ya mto. Tunatakiwa kutumia utaalamu uliopo, kwa sasa mambo ni rahisi nimeona vijana wana teknolojia nyingi za uvunaji maji ya mvua tofauti na miaka ya nyuma,” amesema Rais Dkt. Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amemuagiza Waziri ya Maji, Mhe. Jumaa Aweso kuanzisha Gridi ya Maji ya Taifa kama ilivyo Gridi ya Taifa ya Umeme. Amesema lengo ni kuwa na vituo vya kupokea maji kutoka vyanzo mbalimbali nchi nzima kwa kuweka vituo vya kanda kisha kuwa na utaratibu wa kusambaza maji nchi nzima.