*Arusha
Imeelezwa kuwa Sekta ya Madini nchini Tanzania inaendelea kuwa mhimili wa uchumi wa Taifa, na kukua kwa kasi kutokana na mikakati thabiti ya Serikali kupitia Wizara ya Madini yaliyopelekea kuongezeka kwa ufanisi na mchango wa Sekta katika uchumi wa taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa leo Machi 23, 2025 na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, wakati akifungua Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Madini kilichofanyika katika Ukumbi wa Corridor Spring Hotel jijini Arusha.
Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa mafanikio makubwa yaliyopatikana yametokana na mikakati madhubuti inayotekelezwa na Wizara ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa katika Pato la Taifa, huku Serikali ikiwekeza nguvu kubwa katika kuimarisha ukuaji wake na kuhakikisha madini yanazalisha faida zaidi kwa wananchi.
Amesema kuwa, Serikali imejipanga kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa na matokeo chanya kupitia maono ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, mpango unaolenga kuendeleza Sekta kwa kuongeza utafiti wa kina wa rasilimali madini, kuwezesha wachimbaji wadogo, wa kati, na wakubwa, pamoja na kuhakikisha usimamizi bora wa rasilimali hizi unaleta tija kwa Taifa.
Ili kuhakikisha Watanzania, hususan vijana, wananufaika zaidi na sekta ya madini, Wizara imeanzisha mpango wa Mining for Better Tomorrow (MBT). Mpango huo utawapa vijana nafasi za ajira, mafunzo maalum ya utafutaji na uchimbaji wa madini, pamoja na kuwapatia vifaa vya kisasa vya uchimbaji.
“Vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, na kupitia mpango huu, tutahakikisha wanapata nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika sekta ya madini, siyo tu kama wafanyakazi, bali pia kama wajasiriamali na wawekezaji wa baadaye,” amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Dkt. Kiruswa amefafanua kuwa, ili kuhakikisha madini yanachangia zaidi katika uchumi, Wizara imejipanga kuongeza utafiti wa kina wa madini kutoka asilimia 16 ya sasa hadi kufikia asilimia 50 ya eneo lote la nchi ifikapo mwaka 2030. “Tunataka kubaini maeneo yote yenye rasilimali madini kwa usahihi zaidi, ili kuwezesha wachimbaji wadogo, wa kati, na wakubwa kufanya kazi kwa uhakika badala ya kubahatisha,” amefafanua Dkt. Kiruswa.
Kwa hatua hiyo, wachimbaji wadogo wataweza kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi, huku Serikali ikipata mapato ya kutosha kwa ajili ya kuimarisha sekta nyingine muhimu za kijamii kama afya, elimu, na miundombinu.
Dkt. Kiruswa amewataka wadau wote wa sekta ya madini kushirikiana na Serikali katika kuboresha na kuendeleza sekta hii kwa manufaa ya wote. “Michango yenu ni muhimu sana katika kuhakikisha tunatimiza malengo tuliyojiwekea kwa mwaka 2024/2025 na pia katika kupanga mipango ya 2025/2026 kwa ufanisi zaidi,” amehimiza Dkt. Kiruswa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema kuwa, kwa mujibu wa takwimu za Wizara, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umeongezeka hadi kufikia asilimia 9.0 mwaka 2023, huku kasi ya ukuaji ikifikia asilimia 11.3 katika kipindi hicho. Hatua hiyo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo Sekta hii ilikuwa ikichangia kwa kiwango cha chini zaidi.
Mbibo amesisitiza kuwa mbali na mchango huo, mapato ya Serikali kutokana na maduhuli yatokanayo na shughuli za madini yameendelea kuimarika huku akitolea mfano kuwa, katika kipindi cha Julai 2024 hadi Februari 2025, makusanyo yamefikia shilingi bilioni 690.76, ongezeko la asilimia 42.04 ikilinganishwa na shilingi bilioni 486.30 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Aidha, Mbibo ameongeza kuwa, thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi pia imeongezeka kwa kasi, ikifikia dola za Marekani milioni 3,551.4 mwaka 2023, kutoka dola milioni 3,395.3 mwaka 2022. Ongezeko hilo la asilimia 4.6 linaonesha jinsi sekta hii inavyoendelea kuwa tegemeo la mapato ya kigeni kwa Tanzania. Kwa sasa, madini yanachangia asilimia 56.2 ya mauzo yote ya bidhaa zisizo za asili nje ya nchi, jambo linaloifanya sekta hii kuwa mojawapo ya sekta zenye mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa.
Naibu katibu Mkuu Mbibo ameongeza kuwa, mbali na ongezeko la mapato na uwekezaji, Wizara ya Madini imefanikiwa kutekeleza miradi mingine muhimu, ikiwa ni pamoja na:
Ununuzi wa mitambo 10 ya uchorongaji (rigs) kwa ajili ya kuwezesha wachimbaji wadogo kupata madini kwa urahisi na kwa teknolojia ya kisasa.
Utoaji wa leseni kubwa ya uchimbaji wa madini ya kinywe (SML) kwa Kampuni ya EcoGraf Limited, inayofanya kazi katika eneo la Epanko, Wilaya ya Mahenge – Morogoro.
Pamoja na kukamilika kwa utafiti maalumu na kuchora ramani ya jiolojia ya visiwa vya Zanzibar (Unguja na Pemba) ili kubaini fursa zaidi za madini katika eneo hilo.