Na Ashrack Miraji Michuzi Tv
Wakazi zaidi ya 300 wa kitongoji cha Makei, kijiji cha Bangalala, kata ya Bangala wilayani Same, wameondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi, hali ambayo imewasumbua kwa zaidi ya miaka 20. Hali hii inajitokeza baada ya Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutekeleza mradi wa maji wenye thamani ya shilingi milioni 63.
Wananchi wa kitongoji hicho walionyesha furaha yao baada ya Mkuu wa wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, kuzindua mradi wa uboreshaji wa kisima cha maji Makei, ambapo aliwashauri kuhakikisha wanapokuwa wanatumia huduma ya maji, wanailipa bili pamoja na kulinda miundombinu ili kuzuia hujuma na kuhakikisha mradi unadumu kama ulivyokusudiwa.
“Mlinzi wa kwanza wa miundombinu ya maji ni ninyi wenyewe. Kila mmoja awe mlinzi wa miundombinu hii kwa sababu kila mmoja anahitaji maji. Tuhakikishe tunalipa bili za maji ili fedha zitakazopatikana zitumike kurekebisha miundombinu inapoharibika, hivyo huduma iwe endelevu,” alisema Mhe. Kasilda Mgeni.
Aidha, Mhe. Kasilda alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti kwenye maeneo ya mradi ili kuhakikisha uoto wa asili unaendelea kuwepo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kasilda alimuishukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza sera ya “Kumtua Mama Ndoo Kichwani,” ambayo inalenga kufikisha huduma ya maji kwa wananchi katika maeneo ya vijijini.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Same, Bwana Mbayani Said, alisema kuwa mradi wa maji wa Makei umegharimu milioni 63 za Kitanzania na unahudumia kaya 90 zenye wakazi zaidi ya 360.
Diwani wa kata ya Bangala, Kassim Mnyone, akizungumza kwa niaba ya wananchi, alisema mradi huo ni mkombozi kwa jamii ya Makei, ambayo imekuwa ikikumbwa na uhaba wa maji kwa miaka mingi. Alisisitiza kuwa wananchi watahakikisha wanatunza mradi huo pamoja na uoto wa asili ili kulinda mazingira.