Mratibu wa huduma za afya manispaa ya Sumbawanga Dkt Salum Jipembaakitoa akitoa elimu ya homa ya nyani
Baadhi ya wafanyabiashara wakipatiwa elimu ya ugonjwa wa homa ya nyani
…………………..
Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa :Katika kuhakikisha Jamii inakua salama dhidi ya magonjwa ya kuambukiza, wataalamu wa Afya ya Msingi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga wamewafikia wafanyabiashara na maafisa usafirishaji katika maeneo ya mjini sumbawanga na kuwapatia elimu dhidi ya ugonjwa wa Mpox ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Akizungumza leo March 24 mratibu wa huduma za afya manispaa ya Sumbawanga Dkt Salum Jipemba amewataka maafisa wasafirishaji kuchukua tahadhari kwa kuwa wao ndio wanakutana na watu wengi.
Dkt Jipemba amesema kuwa ili kujikinga na ugonjwa huo ni muhimu maafisa hao wakazingatia kanuni za usafi
“Kwenye vyombo vyenu hakikisheni Kuna vitakasa mikono na maji vitakavyowasaidia abiria kunawa mikono na kubaki salama kwa kuwa mzunguko wa pesa ni mkubwa sambamba na mwingiliano wa watu tofauti unaowabeba”amefafanua Dkt Jipemba.
Akitolea ufafanuzi kuhusu dalili za ugonjwa huo Dkt Jipemba amesema moja ya dalili kubwa ni kupata vipele vinavyotoa maji ambayo mtu mwingine akiguswa na maji hayo anapata maambukizi ya ugonjwa wa homa ya nyani.
“Dalili za ugonjwa huu ni homa ,maumivu ya kichwa ,misuli na mgongo,uchovu wa mwili,kuvimba mitoki ya mwili na vidonda vya koo.
Aidha ugonjwa huo unasambazwa kwa njia mbalimbali kama kula au kugusa mizoga ya wanyama pori walioambukizwa nyani,tumbili, sokwe,na swala wa misituni.
“Sambamba na hilo pia ugonjwa huo unasambazwa na mtu mwenye dalili z ugonjwa huu,kugusa vitu alivyotumia mgonjwa kugusa majimaji ya mwili na kujamiiana na mtu mwenye maambukizi ya mpox “amefafanua Dkt Jipemba
Amesisitiza kuwa wananchi waache mazoea ya kuchangia vifaa mbalimbali ikiwemo mashuka ,vijiko, taulo vyombo vya chakula kugusana kimwili na kugusa mizoga ya wanyama.
Kwa upande wake mwenyekiti wa bajaji manispaa ya Sumbawanga Clement Makundi amesema watahakikisha wanakua na vitakasa mikono, kuacha kushikana mikono, kunawa kila mara, kuepuka kukumbatiana sambamba na kuwa walimu kwa wengine kuhusiana na ugonjwa huo.
“Tutazingatia tahadhari zote tulizopewa ili tusipate maambukizi kwa kuwa sisi tunakutana na watu wengi tunapokea pesa bila kujua imetoka kwa mtu ambae ni salama au la hivyo tutahamasishana sisi kwa sisi na kutoa elimu hii kwa wengine” amesema makundi.
Baadhi ya wafanyabiashara na Maafisa usafirishaji (bodaboda na bajaji) akiwemo Stephano Nicholaus ameliambia mwananchi kuwa wataalamu wa afya waendelee kutoa elimu hii ili iwafikie watu wengi zaidi kwa kuweka mabango na kugawa vipeperushi vitasaidia Jamii kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa homa ya nyani.
“Kila mmoja anapaswa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Mpox kwa kuzingatia kanuni za afya na kuacha utamaduni wa kupeana mikono.
Bado hakuna kisa chochote cha mshukiwa wa ugonjwa huo isipokuwa tahadhari inatolewa ili wananchi hasa wale ambao wanakutana na watu wengi maeneo tofauti tofauti kupatiwa elimu ukizingatiwa mkoa wa Rukwa umepakana na nchi jirani za Zambia na Kongo ambapo visa hivi hutokea huko.
Ikumbukwe kuwa ni mpango wa serikali kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli za biashara katika hali ya usalama wa afya kwa maendeleo endelevu ya jamii na taifa kwa ujumla.