Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo tarehe 24 Machi, 2025.
Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Anna Lupembe akihitimisha Kikao cha kupokea taarifa iliyowasilishwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kuhusu Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 kilichofanyika katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo tarehe 24 Machi, 2025.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja wakifuatilia Kikao cha kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo tarehe 24 Machi, 2025.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira wakifuatilia Kikao cha Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja aktoa ufafanuishiriki kikao cha kuwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo tarehe 24 Machi, 2025.
……….
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema iko katika hatua za kuandaa mfumo jumuishi wa kiutendaji wa usimamizi wa shughuli za mazingira nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira jijini Dodoma leo tarehe 24 Machi, 2025.
Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2024/25 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2025/26 kwenye kamati hiyo, Mhandisi Masauni amesema hatua hiyo utakaowezesha mifumo yote inayohusika na uratibu wa shughuli za mazingira nchini kusomana.
Hatua ya kuandaa mfumo huo ni utekelezaji wa Maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24.
Aidha, akiendelea kuwasilisha taarifa hiyo Waziri Masauni amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendelea na jitihada za kuongeza fedha za ndani kwa kuandika maandiko ya miradi ya mazingira.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/25, Ofisi imeratibu uandaaji wa maandiko dhana ya miradi 17 ikiwemo inayohusu matumizi ya nishati safi ya kupikia na teknolojia zake, wa Urejeshaji wa ardhi iliyoharibika katika maeneo kame na kuzuia mmomonyoko wa ardhi katika maeneo ya milima na miinuko,.
Mhandisi Masauni ametaja miradi mingine kuwa ni kuhimili athari za mafuriko kwenye maeneo hatarishi, usimamizi endelevu wa taka ngumu, udhibiti wa viumbe vamizi, kujenga uhimilivu katika maeneo ya pwani, tathmini ya fursa za biashara ya kaboni na kujenga uwezo wa kitaasisi kutafuta fedha za mabadiliko ya tabianchi.
Hivyo, amesema katika kuwezesha upatikanaji zaidi wa fedha za ndani, baadhi ya maandiko yatawasilishwa Tume ya Mipango kwa ajili kujumuishwa kwenye mipango ya kupata fedha za ndani.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Mhe. Anna Lupembe amepongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utekelezaji wa miradi katika maeneo mbalimbali nchini.
Ametolea mfano Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa Chakula katika maeneo ya Ukame (LDSF) unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora ambao Kamati ilitembelea hivi karibuni.
Amesema mashine za kuchakata mazao ya asali zilizotolewa katika halmashauri hiyo kupitia mradi huo zitasaidia wananchi kujikita katika shughuli za urinaji asali na kuachana na uharibifu wa mazingira.
Pamoja na pongezi hizo, Mhe. Lupembe amehimiza watendaji kuwa na usimamizi wa karibu katika miradi yote inayotekelezwa katika halmashauri zinazonufaika na miradi hiyo .
Mhe. Lupembe ambaye pia ni Mbunge wa Nsimbo amemesema ni muhimu kuisimamia miradi kwa ukaribu ili ikamilike kwa wakati na ilete manufaa kwa wananchi hususan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Pia, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ameshauri kuwa wananchi wanaopelekewa miradi ya mazingira wapatiwe elimu ya namna ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kupanda miti na kusimamia badala ya kuikata.