FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Katika jitihada za kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari na kuhakikisha matumizi sahihi ya mashine za EFD, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Ulanga imeendesha semina ya elimu ya mlipa kodi kwa Kampuni ya Kilombero Valley Teak Company.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Meneja wa TRA Wilaya ya Ulanga, Bw. Abbas Salum, alisisitiza umuhimu wa kampuni kutoa risiti sahihi kila wanapofanya biashara za mazao ya misitu. Alibainisha kuwa utoaji wa risiti za EFD ni hatua muhimu katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji katika ulipaji wa kodi nchini.
“Ni wajibu wa kila Mtanzania kudai na kutoa risiti kwa kila muamala wa kibiashara. Hii inasaidia katika kuongeza mapato ya serikali na kukuza maendeleo ya taifa letu,” alisema Bw. Salum.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi wa Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Morogoro, Bi. Emaculate Chagu, alisema kuwa semina hiyo ni sehemu ya kampeni ya TRA Mkoa wa Morogoro katika kutoa elimu kwa makundi yote juu ya umuhimu wa kutoa risiti na kulipa kodi kwa hiari.
“Tunaendelea na kampeni hii ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanapata uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kulipa kodi na kutoa risiti. Hii itasaidia katika kuongeza uwazi na kuimarisha uchumi wa nchi yetu,” alisema Bi. Chagu.
TRA inaendelea na jitihada zake za kutoa elimu kwa walipakodi katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wadogo na wa kati, ili kuhakikisha kuwa kila mmoja anatimiza wajibu wake wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa.