Na. Abel Paul, Jeshi la Polisi Arusha.
Ujumbe kutoka Idara ya Utalii na mambo ya kale Zanzibar katika kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa wageni na watalii wanaofika nchini kwa ajili ya mapumziko na utalii wamefika Jijini Arusha kwa lengo la kujifunza katika kituo cha Polisi utalii na Diplomasia namna wanavyofanya kazi na kutoa huduma kwa wageni hapa nchini.
Akiongea mara baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika katika kituo cha Utalii na Diplomasia Arusha Mkurungenzi wa Idara ya Utalii na Mambo ya kale Zanzibar Daktari Abdallah Mohamed amesema kuwa moja ya mtaji mkubwa katika biashara ya utalii ni ulinzi na usalama wa eneo husika ambapo amebainisha kuwa mafunzo hayo yamewapa dira na namna ya Kwenda serikali ya mapinduzi Zanzibar kuboresha utendaji kazi wao.
Dkt Mohamed ameongeza kuwa wamekuja Arusha kwa sababu ya uwepo wa kituo hicho cha mfano katika kutoa huduma kwa watalii na wanadiplomasia wanaofika nchini kwa shughuli mbalimbali ambapo amesisitiza kuwa mafunzo hayo yamewajenga na kuongeza mbinu katika utendaji bora.
Aidha Dkt Mohamed akaweka wazi kuwa walipata maagizo kutoka kwa Rais wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar kufika na kuona namna ambavyo kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia Arusha wanavyofanya kazi ili kuwajengea uwezo katika kutoa huduma bora kwa wageni wanaofika Zanzibar.
Kwa upande wake Mkuu wa Operesheni na Mafunzo kutoka kamisheni ya Polisi Zanzibar Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Mathias Nyange amesema wamepata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yakiwemo kutoa huduma bora kwa watalii na wageni wanaofika nchini kwa ajili ya utalii na mapumziko huku akikipongeza kituo cha Utalii Polisi na Diplomasia Arusha kuwa kituo cha mfano.
Nae Mkuu wa kikosi cha Ulinzi wa watalii Zanzibar Kaptain Juma Salehe amesema wamefika kuona na kujifunza ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa idara hiyo ya utalii Zanzibar huku akiweka wazi kuwa kasoro ambazo wamezigundua wanakwenda kuzifanyia kazi ili kutoa huduma bora zaidi kwa watalii.
Mkuu wa kituo cha Polisi Utalii na Diplomasia Mrakibu wa Polisi (SP) Waziri Tenga amesema kuwa ujio wa wageni hao kutoka Zanzibar ni mwendelezo wa mafunzo kwa vitendo kutoka idara na taasisi zinazojihusisha na utalii hapa nchini wanaofika kituoni hapo ambapo ameweka wazi kuwa anamshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuendelea kutoa fursa kwa askari wa kituo hicho kupata mafunzo ndani na nje ya nchi ili kuwajengea uwezo watendaji wa kituo hicho.