Na Mwandishi wetu, Mirerani
WADAU wa maendeleo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kuchangia maendeleo kwa jamii inayowazunguka ili kipato wanachokipata kinufaishe kupitia rasilimali hizo.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Fakii Raphael Lulandala ameeleza hayo mji mdogo wa Mirerani, kwenye iftar aliyoiandaa kwa ajili ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo, wadau wa maendeleo, viongozi wa madhehebu mbalimbali, watoto yatima na wajane.
Lulandala amesema wadau wa maendeleo wanapaswa kuchangia maendeleo ya maeneo waliopo ikiwemo kufanikisha miundombinu ya shule, kununua madawati au sekta ya maji.
Amesema wanapaswa kuchangia ili watoto wa maeneo hayo wanufaike na rasilimali hiyo na kuepukana na watoto wenye uhitaji maalum wanaokosa huduma mbalimbali za lazima kwa jamii.
“Wasichoke kutoa kwa jamii inayowazunguka kupitia mwezi huu wa toba na iftari hii iliyoandaliwa, wakumbuke kutoa wanachopata kwa kusaidia jamii inayowazunguka,” amesema Lulandala.
Amesema watoto yatima, wenye uhitaji na wajane wamepatiwa mbuzi wawili, kondoo mmoja, mchelel kilo 50, sukari kilo 50 mafuta lita 20, maji katoni tano na sharubati katoni tatu, ili kusherehekea sikukuu ya iddi.
Sheikhe wa wilaya ya Simanjiro, Ramia Isanga amesema ni vyema wadau wa madini kuchangia maendeleo kwani haiwezekani uvune magunia kisha usitoe kidogo kwa wengine.
Paroko msaidizi wa kanisa katoliki parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu, Padri Krisantus Asenga amesema chakula hicho kimewaunganisha wote, kwani hata wakristo hivi sasa wamefunga kwaresma.
Mwenyekiti wa madhehebu ya kipentekoste mchungaji Simon Mwita amesema wadau wa madini wanapaswa kuchangia jamii kwani hata vitabu vya dini vimeelekeza watoe sadaka.
Mdau wa maendeleo wa Simanjiro, Lengai Ole Makoo ambaye ameshawahi kujenga madarasa kwenye shule ya msingi Sukuro amesema suala la kuchangia mandeleo kwa jamii halikwepweki.
“Mimi ni mchimbaji wa madini ya Tanzanite hapa Mirerani, japokuwa sijafanya uzalishaji kwa muda mrefu ila nimekuwa nawasisitiza wadau wanapopata wachangie,” amesema Ole Makoo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer amempongeza DC Lulandala kwa kuandaa chakula hicho cha usiku ambacho kimewaunganisha watu wa madhehebu tofauti.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amesema DC Lulandala amefanya jambo jema mno kwani ameunganisha makundi mbalimbali kupitia Iftar hiyo.