Viti vya kukalia abiria vitakavyowekwa kwenye Meki ya Mv.Mwanza

Kaimu Mkurugenzi wa TASHICO Amina Ntibampema akizungumza na waandishi wa habari

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza baada ya kupokea viti vya abiria katika Meli ya Mv.Mwanza.

Picha ya pamoja baada ya kupokea viti
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza unaelekea kukamilika baada ya kuwasili kwa shehena za viti vya kukalia abiria vitakavyofungwa kwenye meli hiyo hatua itakayosaidia kukamilika Mei, 31 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa Jana na Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Amina Ntibampema wakati wa mapokezi ya samani za Meli ya MV. Mwanza katika Bandari ya Kusini Jijini Mwanza.
Alisema kukamilika kwa Meli hiyo kutaongeza tija kiuchumi katika mkoa na abiria ambao wamekuwa wakiwahudumia muda wote katika ziwa Victoria.
“Leo tumepokea Kontena tisa za awali ambazo ndani yake Kuna viti vya kukalia abiria na tunasubili shehena nyingine ya vitanda”, Amesema Ntibampema
Akipokea shehena hiyo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi alisema Serikali imeshatoa zaidi ya bilioni 115.9 sawa na asilimia 93.5 ya gharama ya matengenezo kwa meli hiyo itakayochochea sekta ya kibiashara katika ukanda huu.
Makilagi alisema kuwa serikali ya Awamu ya Sita ilipokea mradi huo ukiwa chini ya asilimia 40 huku mkandarasi akiwa amelipwa asilimia 30 hivyo kutokana na dhamira kubwa ya kuhakikisha utengenezaji wa meli hiyo unakamilika mapema serikali imeendelea kutoa fedha kukamilisha utengenezaji huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 96.
Serikali ya Awamu ya Sita kuanzia mwaka 2021 mpaka 2024 imeleta katika mkoa wa Mwanza zaidi ya trilioni 5.6 ambazo zimetumika katika kugharamia miradi mbalimbali ya kimaendeleo ambayo imeleta matokeo chanya.
Naye Meneja wa Mradi huo, Vitus Mapunda alisema kuwa ujenzi wa meli hiyo umeanza mwaka 2020 hata hivyo kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa virus vya Korona ulisababisha kuchelewa kwa kazi hiyo kutokana na kushindwa kuletwa kwa baadhi ya vifaa vya kutengenezea.
Alisema viti hivyo vilivyowasili vitatumiwa kufungwa kwenye daraja la kwanza, pili, tatu na daraja la uchumi ili kuwezesha wasafiri kusafiri katika mazingira mazuri.
Mapunda alisema meli hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 ya mizigo na gari 20 kubwa na tatu ndogo itawezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kwa uhakika.