Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Luteni Jenerali Salum Haji Othman amempokea na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu la Afrika ya Kusini Luteni Jenerali Sizakele Charmin Mbatha ofisini kwake Upanga Jijini Dar es Salaam tarehe 24 Machi 2025.
Katika mazungumzo yao, Luteni Jenerali Othman amemthibitishia Mgeni wake kuwa JWTZ litaendeleza mahusiano mema yaliyopo hususani katika nyanja za oparesheni na mafunzo baina ya nchi hizi mbili ili kuwajengea weledi na utayari makamanda na wapiganaji kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiulinzi na majanga .
Naye, Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu la Afrika Kusini Luteni Jenerali Sizakele Charmin Mbatha amelishukuru JWTZ kwa mchango wake katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika ikiwemo Afrika ya Kusini. Amesema Afrika ya Kusini inaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Majeshi ya nchi mbili hizi hususan katika nyanja ya Diplomasia ya Ulinzi.
Luteni Jenerali Mbatha na ujumbe wake wapo nchini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya kawaida.