Na Pamela Mollel, Arusha
Arusha, Machi 25, 2025 — Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Said Johari, ametoa wito maalum kwa Mawakili na Wanasheria wote wa Serikali kuzingatia ubora na weledi katika utoaji wa huduma za kisheria, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa wakati ili kuchochea maendeleo ya Taifa.
Akizungumza jijini Arusha katika mafunzo ya pili ya mwaka kwa Mawakili wa Serikali, Mhe. Johari alieleza kuwa ucheleweshaji usio wa lazima katika utoaji wa huduma umekuwa ni changamoto kubwa kwa nchi nyingi za Afrika, na Tanzania haiwezi kukwepa kuathirika endapo haitachukua hatua madhubuti.
“Kaulimbiu yetu ni weledi na ubora, lakini hayo hayawezi kufikiwa kama hatufanyi kazi kwa haraka na kwa wakati. Ugonjwa huu wa kuchelewa chelewa ni tatizo kubwa – unaturudisha nyuma kama Taifa,” alisema Mwanasheria Mkuu huyo kwa msisitizo.
Johari aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuongeza umahiri wa wataalamu wa sheria katika utendaji kazi wao wa kila siku, huku lengo kuu likiwa ni kuleta matokeo yenye tija kwa wananchi kupitia huduma bora za sheria zinazotolewa kwa wakati.
“Tunataka kuacha tabia ya kuahirisha mambo bila sababu za msingi. Tabia hiyo huwanyima wananchi haki zao kwa kuchelewa kupata huduma wanazostahili. Lazima tubadilike,” alisema.
Akitazama mbele, Johari alisema Tanzania inalenga kufikia uchumi wa kati wa viwango vya juu ifikapo mwaka 2050, jambo ambalo haliwezi kufanikiwa kama sekta ya sheria haitaimarika katika kasi na ubora wa huduma zake.
Kwa upande wake, Mwandishi Mkuu wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo hayo, Rehema Katuga, alifafanua kuwa ofisi hiyo ina jukumu pana la kuishauri Serikali kwenye masuala yote ya kisheria.
Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na ushauri kuhusu mikataba, manunuzi ya umma, uandishi wa sheria, pamoja na uangalizi wa utekelezaji wa sheria mpya zinazotungwa.
“Mafunzo haya yamekuja wakati muafaka, hasa ikizingatiwa kuwa tunakutana na changamoto kama kuvunjika kwa mikataba, ambayo mara nyingi husababishwa na mapungufu katika maandalizi au utekelezaji wake. Tunahitaji ujuzi wa hali ya juu ili kukabiliana na changamoto hizi kwa ufanisi,” alisema Katuga.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Said Johari akizungumza jijini Arusha katika mafunzo ya pili ya mwaka kwa Mawakili wa Serikali