Kamati ya ushauri ya mkoa wa Njombe ( RCC ) ikiongozwa na mkuu wa mkoa huo Anthony Mtaka kimepokea na kupitisha pendekezo la kuligawa Jimbo la Ludewa na kuruhusu mchakato huo kuendelea kwa hatua zinazofuata
Awali akiwasilisha taarifa ya kuligawa Jimbo hilo mwanasheria wa halmashauri hiyo Mathani Chalamila amesema kwa asilimia kubwa wamekidhi vigezo vya kuligawa Jimbo hilo ikiwemo ukubwa na jiografia yake kuwa ngumu.
“Mheshiwa mwenyekiti moja kati ya vigezo vya kugawa majimbo ni ukubwa wa eneo wa Jimbo husika ambapo ludewa ina eneo la kilometa za mraba takribani 8,000”. Alisema Chalamila.
Akichangia hoja hiyo mwenyekiti wa CCM mkoa wa Njombe ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Makambako Deo Sanga amesema ni kweli Jimbo la Ludewa linastahili kugawanywa kutokana na ukubwa wa eneo na jiografia yake.
” Chama Cha Mapinduzi huwa tunafanya ziara kule Ludewa, Mheshimiwa mwenyekiti nilikuwa na ombi kwenye kikao chako kuwe na ombi maalum kupitia kikao hiki, hata kama baadhi ya vigezo havikidhi lakini jiografia ya Jimbo hili ni ngumu sana”. Amesema Sanga.
Kupitia kikao hicho Deo Sanga ameomba ombi la kuligawa Jimbo la Ludewa likubaliwe ili waendane na Ilani ya CCM ya kusogeza huduma kwa wananchi.
“Imani yangu Jimbo lile likigawanyika jinsi lilivyo litakuwa limesogeza huduma sana kwa wananchi, yani katika Jimbo kwenye mkoa huu lenye jiografia ngumu ya namna ya kuwahudumia na kuwafikia wananchi ni Jimbo la Ludewa”. Ameongeza Sanga.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Mheshimiwa Wise Mgina sambamba na katibu tarafa wa tarafa ya Liganga Edward Wayotile kwa pamoja wameomba Jimbo la ludewa ligawanywe kutokana na ukubwa wa Jimbo kwani unaweza kutumia muda mwingi kutoka kata moja hadi nyingine kutokana na jografia pamoja na umbali.
Hata hivyo kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka amesema mbali na kuligawa Jimbo kuna haja ya kuanza kufikiria namna ya kuongeza halmashauri katika wilaya hiyo kwani halmashauri ndiyo zinasogeza huduma kwa wananchi kwa ukaribu zaidi.
“Kwahiyo kwangu Mimi tungeiomba serikali iiangalie Ludewa kwa jicho la pili tuombe kupata halmashauri nyingine huko mbeleni”. Amesema Mtaka
Ikumbukwe hatua hiyo imeefikiwa baada ya hivi karibuni Baraza maalum la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa pamoja na kamati ya ushauri ya wilaya hiyo kwa pamoja kulidhia kugawanywa kwa Jimbo hili.