





Na Ali Issa Maelezo 25/3/2025
Wafanyakazi wa Kampuni ya Kurusha Maudhui (ZMUX) wametakiwa kuwa waaminifu na wadilifu katika kazi zao za kila siku ili kuona kampuni hiyo inapiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mkurugenzi Idara ya Uendeshaji na Utumishi Rashid Hamdu Makame katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo wakati wa hafla fupi ya kumuaga aliyokuwa mtumishi wa kampuni hiyo Hawa Ibrahim Saburi amesema uadilifu na uaminifu hufanya mfanyakazi kuwa ni kigezo chema na mfano wa kuigwa katika utendaji kazi.
Amesema mtumishi hufanyakazi kiuadilifu kwa lengo la kutekeleza vyema majukumu yake kwa kutoa huduma bora ili kuinuka kimaendeleo na kuipatia taasisi katika uendeshaji wa huduma zake.
Ameeleza utumishi wa Bi. Hawa Ibrahimu Saburi alikuwa ni mtumishi mwema aliyetukuka katika utekelezaji wa majukumu yake siku zote alizingatia sheria taratibu za kikazi ili kuona sehemu anayofanyia inakwenda vizuri na kuwasisitiza wafanyakazi wa taasisi hiyo kuwa kigezo kwa mama huyo na kufanyakazi kwa ushirikiano na upendo.
Akitoa wasifu wa Mstaafu huyo Afisa Utumishi wa tasisi hiyo Farida Haji Ali amesema Bi Hawa alizaliwa 26/3/1965 Michezani Unguja na alianza elimu ya msingi skuli ya Darajani Mwaka 1972 na kumaliza elimu yake ya sekondari kidato cha nne katika Skuli ya Hamamni mwaka 1982.
Amesema mwaka 1984 Bi Hawa ameajiriwa rasmi katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi katika nafasi ya uhudumu wa ndege na ndani ya kipindi hicho na baadae kuhamishwa katika Taasisi tofaui na kupitia kada mbalimbali katika utumishi wake
Ameeleza kuwa Bi Hawa amefanyakazi katika Idara ya Upigaji Chapa, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Idara ya Tamasha, Mila na Sanaa na amepitia kada ya kuwa karani Kalamazuu, karani fedha, mshika fedha.
Afisa huyo amefahamisha kuwa Bi Hawa alihamishiwa katika Kampuni ya Urushaji Maudhui (ZMUX) Mwaka 2012 akiwa ni mchapakazi mahiri katika utendaji hadi sasa kumalizia utumishi wake Serikalini.
Nae Mstaafu huyo Bi. Hawa Ibrahimu akitoa shukurani zake aliwaasa wafanyakazi kufanyakazi kwa ushirikiano na kupendana ili kufanikisha jukumu waliopewa pamoja na kuwataka kuwa waaminifu na wabunifu siku zote na kusaidiana pale mmoja wao anapohitajia msaada.