Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, akizungumza na wanachama na Viongozi mbalimbali wa CCM wakati akihitimisha ziara yake ya kukagua uhai wa chama pamoja na Maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025 katika ukumbi wa ELCT halmashauri ya Manispa ya Bukoba.

Viongozi na Wanachama wakifuatilia hotuba ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, wakati akihitimisha ziara yake ya kukagua uhai wa chama pamoja na Maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020-2025, katika ukumbi wa ELCT halmashauri ya Manispa ya Bukoba .
………..
Na Mwandishi Wetu, Ngara
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema anazo taarifa za baadhi ya wanachama wanaotaka ubunge kuanza kunja maadili katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Hivyo amewakumbusha wanaotaka ubunge na wabunge waliopo, kuzingatia maadili huku akitoa rai kwa wajumbe wa Chama ambao watapiga kura kuchagua mgombea mmoja kati ya watatu ndani ya Chama kuhakikisha wanapiga kura kwa uhuru bila kupewa fedha na wataka ubunge.
Akizungumza na wanachama wa CCM pamoja na wananchi katiKa kikao cha ndaani kilichofanyika wilayani Ngara mkoani Kagera jana, Wasira alisema Chama kimebadilisha utaratibu wa kupata wajumbe wanaopiga kura kupata wagombea wake.
“Huko nyuma hapa Ngara waliokuwa wanapiga kura ni wajumbe 700, lakini kwa sasa ni zaidi ya 10,000 ni wengi maana sasa hivi mabalozi wote wanapiga kura, kwenye kamati zenu za watu wanne kote huko wanapiga kura.
“Kamati za jumuiya zote zinapiga kura, kamati zao za utekelezaji zote zinapiga kura na watu wengine wengi ambao siwezi kuwataja wote. Tunachotaka mjue sababu za mabadiliko hayo kwanza tunatanua demokrasia ndani ya Chama chetu.
“Pia tunataka watu wengi wanaopiga kura watuambie kwa maoni ya wananchi wa Ngara mtusaidie kusema katika watu watatu mmoja katika hawa anamzidi mwengie ili tupate mtu wa kupeperusha bendera ya CCM kati ya hawa watatu, tujue wananchi wanasemaje,” alisema Wasira.
Alifafanua yeye ni Makamu Mwenyekiti na moja ya kazi yake ni kusimamia maadili hususan kwa wanaotaka ubunge kwani wapo ambao wameanza kunyemelea na wananyemelea kwa kuvunja maadili.
“Wajumbe tunataka mpige kura mkiwa watu huru muiambie CCM mkimsimamisha huyu tutashinda bila tabu kama atakavyoshinda Dk. Samia. Naamini kazi hii wajumbe mnaiweza vizuri hivyo tuleteeni wagombea wanaokubalika.
“Lakini wale wanaotaka ubunge baadhi yao nina habari zao wameanza kuvuruga maadili wanataka muwapigie kura kwa hela wanazowapa na Biblia inasema rushwa inapofusha maana yake ni kwamba ukiona mtu anasambaza hela lazima ujiulize kwani hiyo imekuwa huduma?.
“Na hili nalisema kwa wagombea wapya na wabunge waliopo tunachunguza tunajua mwenendo huo, sasa nawaambia acheni kupofusha wajumbe, na ninyi wajumbe na mabalozi wa nyuma 10 mtupe heshima ya kutuletea watu wazuri, ndio wajibu wenu,” alieleza.
Akieleza zaidi mbele ya wana CCM hao wa Ngara, alisema mtu akipewa rushwa hata rangi ya kijani atasema ni bluu kwa kuwa rushwa imemwambia hivyo “na wewe unang’ang’ana kwamba ni bluu wakati ni kijani na rushwa inafanya upigane kwa sababu imepofusha macho yako.”
Alieleza kuwa hata Ngara, wanaosaka ubunge wameshaanza na wengine wameshasogezwa sogezwa, alionya iwapo wana CCM wakichagua watu kwa sababu ya fedha watakuwa wamewachagua kwa makosa.
SIRI CCM KUBAKI MADARAKANI
Wasira alisema vyama vingi vya siasa vilivyofanikisha kupatikana kwa uhuru barani Afrika vimekufam lakini CCM imeendelea kuwepo kwa sababu imejikita na mizizi yake inaanzia chini, kila nyumba 10 kuna kiongozi wa nyumba na ana kamati.
Alifafanua kuwa ndiyo maana CCM imeendelea kuwa imara “Kama Chama hichi kingekuwa kinashikiliwa na sisi huko juu tungeweza kufikiria kipo kumbe hakipo, ndivyo ilivyotokea kwa KANU (chama kilichopigania uhuru Kenya),”
“Chama kilicholeta uhuru wa Kenya hakipo, Zambia hakipo, Uganda hakipo, lakini chama kilicholeta uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) na mapinduzi ya Zanzibar kipo.
“Wenzetu wanatuuliza mbona tumekaa sana, na sisi tunawaambia tulidai uhuru ili kuendesha nchi na sio kwa muda, shabaha yetu ni kuleta maendeleo” alisema.
UTATUZI WA CHANGAMOTO
Kwa mujibu wa Wasira, CCM imeendelea kuzisimamia serikali zake kuhakikisha changamoto za wananchi zinatatuliwa na kwamba wakati mwingie maendeleo husababisha changamoto mpya.
“Wakati tunajitawala hatukuwa na chuo kikuu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilianzia jengo la TANU Lumumba…wasomi waliokuwa wanatoka pale walikuwa wanapewa kazi moja kwa moja. Kulikuwa na kazi hakuna watu, leo tuna vyuo vikuu 40, vinatoa watu wangapi kwa mwaka?.
“Kwa hiyo watu wamesoma lakini kazi ni chache, ni haki yao kusoma maana huwezi kuwanyima elimu. Maendeleo yanazaa matatizo mapya,” alibainisha.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema maendeleo ni pamoja na kuchukua hatua kuyakabili ndio maana Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amebadili mfumo wa elimu kwa kuanzisha elimu ya ufundi stadi ili kuwajengea uwezo wahitimu na kutengeneza fursa za ajira.