Na Silivia Amandius.
Kagera.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba, mkoani Kagera, imeanza kusikiliza kesi namba 7235 ya uhujumu uchumi inayowakabili watuhumiwa wanne wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali yanayohusiana na ukwepaji wa kodi, kinyume na taratibu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kesi hiyo, inayosikilizwa mbele ya Hakimu Mfawidhi Mkazi wa Mahakama ya Bukoba, Janeth Masesa, iliwasilishwa na Wakili wa Serikali, Judith Mwakyosa, ambaye alieleza kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa tisa yaliyotendwa katika tarehe tofauti wilayani Karagwe.
Miongoni mwa makosa yanayowakabili ni pamoja na kuwa na bidhaa zisizosajiliwa, kutengeneza bidhaa bila leseni, kushindwa kuwasilisha maombi au tamko rasmi kwa TRA, kutowasilisha mrejesho wa bidhaa, kushindwa kutunza kumbukumbu, kushindwa kubandika stempu za kielektroniki, kushindwa kulipa kodi inayozidi milioni 10, kusaidia ukwepaji wa kodi, na kusababisha hasara kwa serikali.
Kwa mujibu wa Wakili Mwakyosa, watuhumiwa hao ni Mwesiga Rupia, Nelius Kaizirege, Julieth Ishengoma, na Erieth Gerevaz. Alifafanua kuwa Mwesiga Rupia na Nelius Kaizirege wanakabiliwa na kosa la kushindwa kubandika stempu za kielektroniki, kushindwa kulipa kodi, na kusaidiana katika ukwepaji wa kodi. Aidha, watuhumiwa wa tatu na wanne, Julieth Ishengoma na Erieth Gerevaz, wanatuhumiwa kwa kuhifadhi bidhaa zisizo na stempu, ambapo nyumbani kwa Julieth zilikutwa chupa za pombe aina ya Jagwa bila stempu halali.
Hakimu Masesa alieleza kuwa mahakama imewapa washitakiwa masharti ya dhamana, ambapo Mwesiga Rupia na Nelius Kaizirege wanapaswa kuwa na wadhamini wawili, kila mmoja akiwa na dhamana ya Sh milioni 2.6, pamoja na barua na vitambulisho vya makazi. Endapo watashindwa, wanapaswa kuwasilisha hati ya dhamana ya mali isiyohamishika. Kwa upande wa Julieth Ishengoma na Erieth Gerevaz, wao wanapaswa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho halali na kuhakikisha wanahudhuria mahakamani kila wanapohitajika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 8, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa tena.