
Na Mwandishi wetu, Hanang’
MBUNGE wa Jimbo la Hanang’ Mkoani Manyara, mhandisi Samwel Hhayuma Xaday ameweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa Bassotughang utakaonufaisha watu 4,995 wa kata ya Hidet.
Watu hao watanufaika kupitia mradi huo wa maji kutoka ziwa Bossoutghang baada ya kujengwa kwa mitambo ya kusafisha maji hayo na kuanza kutumika kwa matumizi ya binadamu hivyo kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji
Mhandisi Hhayuma ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuwakumbuka wananchi wa eneo hilo kwa kuwawekea miundombinu bora ya upatikanaji wa maji.
Hhayuma amesema mradi huo umewashinda viongozi wakubwa waliokuwa wanaongoza wilaya hiyo kwa muda mrefu hadi kukamilika kwake mwaka huu wa 2025.
“Kuna wazee niliwaambia huu mradi wa maji wa Bassotughang utafanikiwa wakaniambia sitaweza kwani watangulizi wangu viongozi wakubwa walishindwa,” amesema Hhayuma.
Amesema pamoja na mradi huo amefanikisha kukamilisha mradi wa maji mji mdogo wa Katesh ambao baadhi ya watu walikuwa wanachota maji kwa kuvuta na kutumia punda.
“Tunamshukuru Mungu hivi sasa suala la maji limekuwa historia kwani watu wanapata maji na wale wazee walioniambia sitaweza hili wamekuja na kunipongeza,” amesema Hhayuma.
Hata hivyo, amewapongeza wakazi wa maeneo hayo kwa kuvuta subira hadi kufanikisha upatikanaji wa maji.
Meneja wa mamlaka ya maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) wilaya ya Hanang’ Herbet Kijazi amesema mradi huo umegharimu zaidi bilioni Sh1.5 bilioni ambazo ni fedha za serikali kuu.
Kijazi amesema mradi huo wa maji wa Bassotughang utawanufaisha watu 4,995 wa kwenye kata ya Hidet.