Na Mwandishi Wetu.
Katika jitihada za kumuunga mkono juhudi za Rais wa awamu ya Sita Dk.Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha kielimu watoto wa kike, shule ya Msingi ya Brookside iliyopo Kata ya Kimara ,Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es Salaam ina mpango wa kujenga shule ya sekondari ya wasichana ya bweni Bagamoyo mkoa Pwani.
Shule hiyo ya mchepuo wa Kiingereza iliyopo Kimara Suka inapanga kutekeleza mradi huo kwa lengo la kuboresha maisha ya wasichana hapa nchini.
Mkurugenzi wa Shule hiyo Sia Meena anasema kuwa shule hiyo itajengwa Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Bagamoyo eneo la Saadan kijiji cha Mkuranga .
“Tunajenga shule hiyo ili kumuunga mkono Rais wetu katika kumshika mkono mototo wa Kike ki- elimu’ alisema.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Shuleni hapo, Mkurugenzi huyo alimpongeza Rais Samia kwa kujenga shule za Sekondari za wasichana karibu nchi nzima , kitendo ambacho kimewashawishi wao kama wadau wa elimu kumuunga mkono kwa kujenga shule ya sekondari ya bweni.
Alimpongeza Rais Samia pia kwa uamuzi wake wa kuwarudisha shule wasichana waliopata mimba wakiwa shuleni kwani uamuzi huo ni ukombozi wa mototo wa kike.
Naye Meneja Rasilimali Watu na Utawala wa Shule hiyo Masanja Doto alisema shule ina shirikiana na serikali kwa kutekeleza miongozo mbalimbali ikiwamo sera mpya ya elimu.
Alisema sera hiyo ambayo inatilia mkazo mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi inajenga msingi mzuri kwa wanafunzi kujiajiri pindi wamalizapo masomo yao.
Alisema kupitia sera hiyo watoto wanafundishwa standi mbalimbali za kazi kama kilimo, upishi, ushonaji na muziki.
“Sisi hapa tuna darasa la muziki kama unavyojua muziki ni ajira, muziki unaajiri vijana wengi sana na unaliingizia taifa mapato, nitoe rai kwa wazazi kuwaleta watoto wao hapa kwa ajili ya kupata ujuzi wa fani mbalimbali,”
Frank Kalenga ambaye ni Mwalimu wa Taaluma alisema shule imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma karibu kila mwaka. Mfano alisema kwa mwaka 2023 wahitimu 70 wa darasa la saba, walipata alama 272 ambazo ni ufaulu wa daraja A bora.
Mwaka 2024 wahitimu wa darasa la saba 107 walipata alama 286.33, 106 wakipata daraja A bora na moja alipata wastani wa alama B.
“Matokeo hayo yanaonyesha ubora wa shule yetu upande wa elimu,” alisema.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Brookside