Na Silivia Amandius
Kagera.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Kagera, Casto John, ametoa ufafanuzi kwa wafanyabiashara kuhusu ukomo wa makadirio ya kodi, huku akisisitiza umuhimu wa ulipaji kodi kwa wakati ili kuepuka adhabu za kisheria.
Kwa mujibu wa Meneja huyo, makadirio ya kodi yanazingatia vigezo kadhaa, ikiwemo aina ya biashara, mauzo yanayofanyika, na rekodi za mapato za mfanyabiashara husika.
Ameeleza kuwa mfumo huu unalenga kuhakikisha haki inatendeka kwa wafanyabiashara wote kwa mujibu wa sheria.
Pamoja na hilo, John amewakumbusha wafanyabiashara kuwa ni lazima kutoa risiti halali kwa kila mauzo wanayofanya ili kuimarisha uwazi na kudhibiti upotevu wa mapato ya serikali.
Aidha, ameonya kuwa mfanyabiashara yeyote atakayekiuka matakwa ya ulipaji kodi, ikiwa ni pamoja na kutotoa risiti au kukwepa kodi kwa namna yoyote, atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Hatua hizo zinaweza kujumuisha faini kubwa au kifungo kulingana na uzito wa kosa.
TRA imeendelea kusisitiza kuwa ofisi zake ziko wazi kwa yeyote anayehitaji ufafanuzi zaidi kuhusu masuala ya kodi, huku ikihimiza wafanyabiashara kushirikiana na mamlaka hiyo kwa maendeleo ya Taifa.