Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Profesa Isaya Jairo (kulia) akiwa na Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Bw. Eric Urio wakipongezana baada ya kutia saini ya makubaliano ya usimamizi wa kozi ya kozi ya Uwakala wa Forodha Afrika Mashariki (EACFFPC) katika hafla iliyofanyika leo Machi 27, 2025 jijini Dar es Salaam
Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Profesa Isaya Jairo (kulia) akiwa na Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Bw. Eric Urio wakitia saini ya makubaliano ya usimamizi wa kozi ya kozi ya Uwakala wa Forodha Afrika Mashariki (EACFFPC) katika hafla iliyofanyika leo Machi 27, 2025 jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Chuo cha Kodi (ITA) na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) wakiwa katika picha ya pamoja.
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Chuo cha Kodi (ITA) kimeingia makubaliano na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) kwa ajili ya usimamizi wa kozi ya Uwakala wa Forodha Afrika Mashariki (EACFFPC) ambayo inatoa fursa ya kuongeza ufanisi kwa mawakala na kufanya kazi ya forodha mahali popote Duniani.
Akizungumza leo Machi 27, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya kutiaji saini ya makubaliano ya usimamizi wa kozi ya EACFFPC kati ya ITA na TAFFA, Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Profesa Isaya Jairo, amesema kuwa makubaliano hayo ni fursa muhimu kwa mawakala wa forodha nchini kujiendeleza ili kunufaika na mafunzo ya uwakala jambo ambalo litasaidia kufanya kazi kwa weledi na kisasa pamoja na kuongeza mapato yanayotokana na forodha.
Profesa Jairo amesema kuwa jumuiya ya Afrika Mashariki inahitaji mawakala wa forodha wenye weledi ambao watapunguza changamoto zinazojitokeza katika tasnia ya uwakala wa forodha.
”Chuo cha Kodi tutatimiza wajibu wetu kuhakikisha TAFFA inaendesha kozi ya EACFFPC kwa weledi na kwa kuzingatia misingi na matakwa ya mtaala pamoja na wadhibiti wa elimu nchini ambao ni Wizara ya Elimu, Baraza la Taifa la Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) ili kulinda ubora wa kozi za ITA na taswira ya TRA” amesema Profesa Jairo.
Amesema kuwa ushirikiano huo utadumu na kupelekea kupatikana fursa nyingine za kushirikiana katika masuala mbalimbali ya forodha ikiwemo utafiti na mazingira bora ya utendaji kazi wa shughuli za forodha ili kulea tija kwa Taifa.
Profesa Jairo amesema kuwa ushirikiano huo huushii katika kusimamia kozi ya EACFFPC, bali kutakuwa na program nyengine za mafunzo katika nyanja za forodha na utawala wa forodha kwa wadau wa TAFFA.
“Tumekuwa mstari wa mbele katika ukanda wa mashariki na kusini mwa Afrika kuwajengea uwezo watumishi wa mamlaka za mapato kutokana na umahiri wa kuwa na wataalam waliobobea katika masuala ya forodha na kodi” amesema Profesa Jairo.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Bw. Eric Urio, amesema kuwa chuo cha kodi ni kiungo muhimu katika uendeshaji wa tasnia ya forodha kwa kuhakikisha wanakuwa na watendaji wenye viwango wa kukusanya kodi pamoja na kujenda ushindani nchi mbalimbali duniani.
“Hii ni hatua kubwa ya ushirikiano ambayo tumeanza na kutegemea ndani ya miaka mitano katika kujengeana uwezo, kunyanyuana katika taaluma pamoja na kuendelea kutuza heshima katika tasnia hii ya Clearing and Fowarding” amesema Urio.