NA WILLIUM PAUL, MOSHI.
MBUNGE wa viti maalum kupitia mkoa wa Kilimanjaro, Zuena Bushiri ameendelea kusapoti Umoja wa Wanawake wa chama cha Mapinduzi(UWT) mkoa wa Kilimanjaro ambapo amekabidhi mabati 50 kwa ajili ya kuezekea nyumba ya Katibu wa mkoa wa UWT.
Hatua hiyo ni kuhakikisha Mtumishi huyo anaishi katika nyumba ambayo itakuwa ni mali ya UWT ambapo mabati hayo amemkabidhi Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kilimanjaro, Elizabeth Minde pamoja na Katibu wake, Erimina Mushongi.
Akikabidhi mabati hayo, Mbunge huyo alisema kuwa, anaunga mkono zilizoanzishwa na UWT kuhakikisha watumishi wake ambao ni Makatibu wa UWT wilaya na mkoa wanapata nyumba.
Aliahidi kuendelea kushirikiana na wanachama wa UWT mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha nyumba hiyo inakamilika mapema na Katibu anahamia hapo.
Akitoa shukrani kwa Mbunge huyo, Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kilimanjaro, Wakili Elizabeth Minde alimshuku Zuena kwa jinsi ambavyo amekuwa akijitoa kuisapoti Umoja huo katika mambo mbalimbali.
“Mbunge Zuena ni mbunge wa kuigwa kwani amekuwa mstari wa mbele kujitoa katika maswala yanayohusu Umoja huo pamoja na chama hivyo nimshukuru sana kwa leo kutukabidhi mabati haya 50 na ametuahidi kuendelea kushirikiana na sisi mpaka ujenzi wa nyumba hii utakapokamilika” Alisema Wakili Elizabeth.