Na Prisca Libaga Arusha.
Katibu Tawala Mkoa wa Arusha(RAS) Mussa Misaile, amewapongeza wanawake na wasichana waliokuwa waraibu wa dawa za kulevya ambao wamejitambua na kutoka kwenye maisha hayo ya kutumia dawa za kulevya .
Ametoa pongezi hizo alipokuwa akifungua Kongamano la Wanawake na Wasichana 2025; Tukatae Dawa za Kulevya, lililofanyika sanjari na kuwakabidhi vifaa vya mama lishe ili wakaanzishe vijiwe vya kupikia na kuuza vyakula kwa watu mbalimbali.
Amesema wanawake ni nguzo ya Taifa kuwapoteza kwa kuwaacha kwenye matumizi ya dawa za kulevya ni athari kubwa kwa Taifa kwa kuwa wao ni nguvu kazi katika shughuli za uchumi hivyo akalitaka Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kuendelea na kudhibiti matumizi ya dawa hizo.
Misaile amesema kuwa zipo changamoto mbalimbali za dawa za kulevya na inahitajika nguvu ya pamoja katika kupambana na dawa za kulevya na DCEA imeanzisha vilabu vya kupambana na dawa za kulevya kwenye shule na vyuo lengo ni kutoa elimu ya madhara ya matumizi ya dawa hizo.
Amesema baadhi ya waraibu wanaingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na ushawishi wa marafiki zao wenye nia mbaya kupitia sigara na vinywaji mbalimbali na wengine wanadai hawana elimu ya madhara ya dawa za kulevya huku wengine wakidai ni matatizo ya kiuchumi na matokeo yake nchi inapata hasara kwa kukosa nguvu kazi ya uzalishaji.
Amesema Arusha zipo nyumba za upataji nafuu 15 (Sober House) zinazowahudumia waraibu zinafanya vizuri sana hivyo akaomba apangiwe ratiba ili azitembee na Serikali itaangalia namna ya kuzisaidia. Misaile, amesema kuwa waraibu wengine wameingia kwenye madanguro na huko ni kuathiri miili wanapata magonjwa na kuathiri uzalishaji akawataka walioacha uraibu wawe ni mabalozi wazuri watoe elimu kwenye shule na vyuo ili watambue athari zisiongezeke.
Afisa Ustawi na Elimu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) Kanda ya Kasikazini, Sarah Ndaba, ameomba Taasisi za Serikali mkoani Arusha waipe mialiko Mamlaka ili wakatoe elimu ya athari ya matumizi ya dawa za kulevya katika Taasisi zao.
Amesema waraibu wengi hawana uwezo wa kugharimia gharama za matibabu kwa kuwa hawana bima za afya hivyo kaomba wadau mbalimbali kuwasaidia gharama za matibabu kwa kuwalipia Bima za Afya Ngazi za Kata ambayo ni shilingi 30,000 kwa mwaka.
Amesema kuwa waraibu wa dawa za kulevya wamekuwa wakisahaulika, hivyo akaomba wadau wasaidie vitanda na matandiko kwa kuwa nyumba nyingi zinazowahifadhi na kuwapatia huduma ya matibabu hazina vitanda.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha (OCD) Georgina Matage amewapongeza walioacha dawa za kulevya anatamani mabinti wote waache kutumia dawa hizo za kulevya na Jeshi la Polisi wanaona matumizi ya dawa za kulevya ni ukatili wa kijinsia .
Amesema mwaka huu Jeshi la Polisi Wilaya ya Arusha limeshatoa vifaa vya saluni kwa waliokuwa waraibu wa dawa za kulevya na leo wamekabidhi vifaa vya mama lishe ambavyo ni masufulia, sahani jiko la gesi ndoo za kunawia na kutupia taka.
Amesema lengo la msaada huo ni kuwawezesha wasirejee tena kwenye matumizi ya dawa za kulevya na hivyo kuwatoa kwenye matumizi ya dawa hizo.
Vifaa hivyo vimetolewa na wadau mbalimbali ambao ni DCEA Kanda ya Kaskazini, Jeshi la Polisi Wilaya, Chuo cha Uhasibu Arusha, Benki ya NMB N. K.









