Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Bw. Crispin Chalamila kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi, 2025.
…………..
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema kuwa ubadhirifu unaoendelea kujitokeza katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri nchini unatokana na ushirikiano wa baadhi ya wasimamizi, wahasibu, na wakusanyaji wa mapato wanaojinufaisha na fedha hizo.
Hayo yamebainishwa leo Machi 27, 2025, na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, wakati akiwasilisha ripoti ya utendaji ya taasisi hiyo kwa mwaka 2023/2024 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Chalamila, ukosefu wa usimamizi madhubuti katika kuhakikisha mapato yanapelekwa benki pamoja na baadhi ya wasimamizi kukosa uadilifu ni miongoni mwa changamoto zinazochochea ubadhirifu huo. “Hivyo ni vema viongozi wa halmashauri wakaimarisha usimamizi kwenye eneo la ukusanyaji wa mapato ya serikali,” amesema.
Katika hatua nyingine, Chalamila ameeleza kuwa TAKUKURU imekamilisha uchunguzi wa majalada 728, ambapo 17 kati ya hayo yanahusisha rushwa kubwa yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 11.
Akitaja baadhi ya kesi hizo, amesema uchunguzi umebaini ukiukwaji wa taratibu katika upangaji wa jengo la Ngorongoro Tourism Center, ambapo kodi ya Shilingi bilioni 7.96 ilipunguzwa bila ridhaa ya Bodi ya Wakurugenzi.
Aidha, uchunguzi umebaini uwepo wa vitendo vya rushwa na utakatishaji fedha wa Shilingi bilioni 4.2 katika kitengo cha Agency Banking cha Benki ya CRDB, ambapo mawakala wakuu (Super Agency) walitoa hongo ili mikataba yao isisitishwe.
Chalamila pia ameeleza kuhusu ubadhirifu wa Shilingi bilioni 2.35 uliofanywa na maafisa wa Benki ya ABC, kwa kutumia mbinu mbalimbali za udanganyifu, ikiwemo miamala ya kurejesha fedha (Teller Reversal Entries) na matumizi mabaya ya huduma za kadi ya malipo ya kabla (pre-paid card services).
Pia, ameibua tuhuma dhidi ya kampuni ya NatGroup Limited, ambayo ilishirikiana na watu wengine kutumia dhamana ya Shilingi bilioni 2.3 kutoka First Assurance kwa njia ya udanganyifu ili kupata mkopo wa kununua petroli kutoka United Petroleum Limited.
TAKUKURU imesisitiza kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote wanaohusika na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye hafla ya kupokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023-2024 pamoja na Taarifa ya Mwaka ya Utendaji Kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ikulu Jijini Dar es Salaam.