Na Rose Ngunangwa
Dunia imehitimisha shamrashamra za Siku ya Kimataifa ya Wanawake, na hata hivyo, tunapoadhimisha mwezi huu maalumu, ukatili wa kijinsia unaendelea kuenea kwa kasi. Si tu kwa wanawake na wasichana, bali pia kwa watoto, wanaume vijana na wazee.
Kila kundi linakutana na changamoto zake katika suala hili. Wadau mbalimbali wanashirikiana katika kukabiliana na tatizo hili, lakini changamoto bado ni kubwa na inashindikana kuondoa tatizo hili kabisa.
Kwa mfano, katika maeneo kama Mgagao, wilayani Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro, ndoa na mimba za utotoni bado zinawaathiri wasichana wengi. Wasichana hao hulazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, kwenda shule ya sekondari Mgagao, na kutafuta kuni za kupikia.
Mwandishi wa habari hizi alifanya mahojiano na Justine Kiverenge, Katibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa cha Mgagao, kinachosimamiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
Kiverenge alieleza kuwa ongezeko la mimba za utotoni linachangiwa na ukosefu wa mabweni ya wasichana katika shule, kama vile Shule ya Sekondari Mgagao.
Hali hii imewalazimu wasichana kutembea umbali mrefu wa kilomita saba kufika shule, jambo linalowaweka katika mazingira hatarishi.
“Kama wawezeshaji kutoka Kituo cha Taarifa na Maarifa, tunahisi kwamba kazi yetu imechangia kupunguza matukio ya ukatili wa kijinsia, ingawa sababu zake bado zipo. Hii ni kwa sababu ya ukosefu wa mabweni, ambapo wasichana wanashindwa kukaa shuleni na badala yake wanatembea umbali wa hadi kilomita saba kufika shule. Katika juhudi zetu, tunajitahidi kuihamasisha jamii kuepuka unywaji wa pombe kupita kiasi,” anasema Kiverenge.
Kwa mujibu wa Kiverenge, wanafunzi wanaoishi katika kijiji cha Pangaro, kwa mfano, wanatakiwa kutembea kati ya kilomita saba hadi nane ili kufika shuleni. Hii inawaweka katika hatari kubwa, kwani barabara wanayotumia inakata katika vichaka vingi na vikubwa.
Hata hivyo, Kiverenge anasema kuwa serikali imetangaza mpango wa kujenga mabweni katika Shule ya Sekondari Mgagao ili kuwaepusha wasichana dhidi ya hatari ya kupata mimba zisizotarajiwa.
Alipoulizwa kuhusu hatua zilizofikiwa katika kubadilisha mila na desturi hatarishi, Kiverenge anakiri kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa, hasa miongoni mwa jamii ya Wamasai. Jamii hii bado huwaoza wasichana wao wakiwa na umri mdogo kwa ajili ya kupata mifugo.
Kuhusu ukeketaji wa wasichana, anasema kuwa huenda bado unafanyika, lakini kwa siri sana, jambo ambalo linachangiwa na kampeni mbalimbali zinazofanywa na asasi binafsi za kiraia na serikali. Serikali pia imeweka sheria kali dhidi ya vitendo hivi, na jamii inafahamu kuwa yeyote atakayekiuka sheria hizi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ripoti ya Benki ya Dunia ya Tathmini ya Hali ya Ukatili wa Kijinsia Tanzania, Tanzania Gender-Based Violence Assessment, imebaini kuwa, ingawa nchi imepiga hatua kuelekea usawa wa kijinsia katika ushiriki wa wavulana na wasichana katika elimu ya msingi, bado kuna pengo kubwa la kijinsia katika ngazi za sekondari na elimu ya juu, hasa maeneo ya bara.
Viwango vya chini vya elimu kwa wasichana vinahusishwa moja kwa moja na mimba za utotoni, uzazi wa mapema, fursa finyu za kiuchumi, na kipato kidogo katika kipindi chote cha maisha yao.
Ingawa Tanzania imefikia usawa wa kijinsia katika elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya juu, bado kuna upungufu mkubwa wa usajili wa wasichana kwa kiwango kikubwa katika ngazi ya sekondari na elimu ya juu.
Hali hii inahusishwa na masuala kama kipindi cha balehe, ndoa na mimba za utotoni, na majukumu ya ziada ya familia, kama inavyobainishwa kwenye ripoti ya Benki ya Dunia.
Kwa ujumla, bado kuna mambo mengi yanapaswa kufanyika ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya mimba na ndoa za utotoni.
Kwa kuanzia, wadau kutoka sekta za umma na binafsi wanapaswa kushirikiana kujenga mabweni katika shule za sekondari ili kupunguza umbali wa kutembea kwenda na kutoka shule.
Hii itasaidia kuwaepusha wasichana na hatari ya mimba zisizotarajiwa na ubakaji.
Aidha, ni muhimu kuishirikisha jamii katika kufanikisha suala hili, kwani jamii inaweza kusaidia kwa njia mbalimbali kama vile ufyatuaji wa matofali, kukusanya mchanga, na kutoa michango ya aina mbalimbali ili kurahisisha ujenzi wa mabweni.
Hakika, tumepiga hatua, lakini ni wazi kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanywa ili kumlinda mtoto wa kike. Tushirikiane kwa pamoja katika kumuelimisha mtoto wa kike na jamii kwa ujumla, kwani yeye ni mama wa baadaye na kiongozi wa jamii zote ulimwenguni.