Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna wakati alipowasili katika Uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB – Chanika Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna wakivuta kitambaa wakati wa uwekaji wa Jiwe la Msingi la Uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB – Chanika Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB – Chanika Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akitembelea maeneo mbalimbali ya utoaji huduma ndani ya jengo la Benki ya NMB – Tawi la Chanika Jijini Dar es Salaam mara baada ya kuzindua Tawi hilo leo tarehe 28 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna pamoja na Viongozi mbalimbali wa NMB katika picha ya pamoja na watumishi wa Benki ya NMB tawi la Chanika Jijini Dar es Salaam mara baada ya kuzindua tawi hilo leo tarehe 28 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB – Kinyerezi Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Machi 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB – Kinyerezi Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Machi 205.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna mara baada ya uzinduzi wa Tawi la Benki ya NMB – Kinyerezi Jijini Dar es Salaam leo tarehe 28 Machi 2025.
…………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema kufunguliwa kwa matawi ya Benki karibu na wananchi kutasaidia kuondokana na wakopeshaji binafsi maarufu kama kausha damu ambao licha ya kutoza riba kubwa, wananyanyasa na kutweza utu kwa vitendo vya ukamataji mali za wadaiwa.
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kuzindua Tawi la Benki ya NMB Chanika na Tawi la Benki ya NMB Kinyerezi Jijini Dar es Salaam. Amesema uzinduzi wa matawi hayo ya Benki utachangia maendeleo ya Taifa kwa kulipa kodi mbalimbali na kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Hali kadhalika, amesema tawi la Benki hiyo litawezesha kufanyika kwa usalama zaidi wa miamala mbalimbali kama vile malipo ya bili za maji na umeme, ada za shule na mauzo ya bidhaa mbalimbali.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Benki ya NMB kuendelea kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo katika sekta ya Afya na Elimu. Amesema uwajibikaji kwa jamii ndio msingi imara wa mahusiano bora na yenye tija kati ya benki na jamii. Aidha ameongeza kwamba kwa kuendelea kuongeza idadi ya mawakala kutasaidia katika kuzalisha ajira kwa vijana ambao ndio wadau wakubwa huduma hizo.
Vilevile, Makamu wa Rais amesema ni vema kuelekeza nguvu zaidi katika kukuza elimu na uelewa kuhusu masuala ya fedha ambao umeonekana kuwa mdogo miongoni mwa wananchi. Ametoa wito kwa Benki ya NMB kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na Umoja wa Mabenki kubuni programu na mikakati zaidi ya kuongeza elimu kwa Watanzania, hususan kwa wale waishio vijijini. Amesema ni muhimu kuangalia namna bora ya kupunguza gharama za huduma za kibenki za kidijiti ambazo baadhi zinaonekana kuwa kubwa na hivyo kukinzana na lengo la Taifa kupunguza matumizi ya fedha taslimu ili kurahisisha malipo, kuchochea matumizi na kuipunguzia Serikali gharama za kutengeneza sarafu.
Aidha Makamu wa Rais amesema Sekta ya Benki na fedha kwa ujumla imeendelea kukua na kuonesha mafanikio makubwa ambayo yanaonekana katika huduma bora zitolewazo. Kadhalika, mchango wake katika ukuaji wa Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 2.3 mwaka 2019 hadi asilimia 8.6 mwaka 2023. Ametoa rai kwa NMB kujizatiti kwa kujiwekea mikakati itakayowajengea utayari na uwezo wa kuhimili mitikisiko inayoikumba dunia ikiwemo ya kiuchumi, magonjwa na vita.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB Bi. Ruth Zaipuna amesema kwa kutambua idadi ndogo ya watumiaji wa huduma za kibenki hususani vijijini, Benki ya NMB imeanzisha mpango mkakati wa kupelekea huduma za kibenki vijijini hususani kupitia uwekezaji wa Wakala na matumizi ya teknolojia. Amesema mpango huo umelenga kuhakikisha kila Kijiji nchini Tanzania kinakuwa na Mawakala angalau wawili wa Benki ya NMB ili kuwasogezea wananchi huduma za kibenki karibu yao.
Aidha amesema Benki ya NMB imeendelea kushiriki katika mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo tayari imetenga zaidi ya shilingi bilioni 100 maalum kwaajili ya miradi na biashara zinazopeleka na kusambaza nishati safi ya kupikia kwa Watanzania.
Kuzinduliwa kwa matawi ya Benki ya NMB – Chanika na Kinyerezi kunaifanya Benki hiyo kuwa na matawi 241 nchi nzima.