Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. Dennis Londo (Mb) amepokea nakala ya Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Jamhuri ya Equatorial Guinea makazi yake nchini Uganda Mhe. Carmelo-Micha Nguema Misi.
Akipokea Nakala ya hati hizo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, katika Ofisi Ndogo za Wizara, jijini Dar es Salaaam Mhe. Londo ampongeza Mhe. Nguema Misi kwa kuaminiwa na kuteuliwa kuiwakilisha nchi yake hapa nchini na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, itampatia ushirikiano wakati wote ili kumwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mhe. Londo amesema uhusiano wa Tanzania na Jamhuri ya Equatorial Guinea umeendelea kuimarika na kuchochea maendeleo kati ya nchi hizo mbili na kuongeza kuwa kuna haja ya kuendelea kuimarisha uhusiano huo kwa kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa vitendo.
“Kuna haja ya nchi kuboresha ushirikiano katika kutekeleza diplomasia ya Uchumi kwa kuibua maeneo mapya ya ushirikiano hususan katika mafuta na gesi, utalii, elimu ya juu na utamaduni kupitia lugha ya Kiswahili” Mhe. Londo alifafanua.
Kwa upande wake Mhe. Nguema Misi amesema Equatoria Guinea iko tayari kuingia hatua ya kuandaa hati za makubaliano ya kuanzisha miradi ya ubia na Tanzania katika sekta za kilimo, utalii, utamaduni kupitia lugha ya Kifaransa na elimu ya juu.