Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, amesema Serikali imejipanga kuboresha ufundishaji wa masomo ya sayansi na hisabati ili kuongeza ubunifu kwa wanafunzi na kuwaandaa kwa mahitaji ya soko la ajira.
Akifunga mafunzo ya walimu wa masomo hayo mkoani Singida, Prof. Mkenda amesema kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), Serikali inawapa walimu mbinu za kisasa ili kuhakikisha wanafunzi wanajifunza kwa ufanisi zaidi.
“Tunahitaji elimu inayochochea fikra tunduizi kwa wanafunzi. Hili linawezekana tu ikiwa walimu watatumia mbinu bora za ufundishaji,” amesema Prof. Mkenda.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo ya Ualimu, Huruma Mwageni, zaidi ya walimu 40,000 wamenufaika na mafunzo hayo katika mikoa yote ya Tanzania, hatua inayolenga kuimarisha ufaulu wa wanafunzi katika masomo ya sayansi na hisabati.
Kwa upande wake, mwakilishi wa TAMISEMI, Singo Yusuph, amesema Serikali inaendelea kufuatilia matokeo ya mafunzo hayo ili kuhakikisha yanaleta tija katika mfumo wa elimu nchini.
Aidha, kupitia Dk. Samia Scholarship, wanafunzi 600 waliomaliza kidato cha sita na kufaulu kwa viwango vya juu wamepata ufadhili wa kusomea masomo ya sayansi katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Godwin Gondwe, amesema mkoa huo unanufaika na miradi kadhaa ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule ya kisasa ya mafunzo ya amali yenye thamani ya bilioni 1.5, ambayo itasaidia wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo sambamba na elimu ya darasani.
Mageuzi haya ni sehemu ya utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), inayolenga kuimarisha ubora wa elimu kwa kuzingatia ubunifu na matumizi ya teknolojia.