Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa: Wajasiliamali wametakiwa kujiunga katika vikundi vitakavyowasaidia kupata mikopo kwa njia rahisi.
Hayo yamesemwa leo March 28,2025 na mbunge wa viti maalumu mkoa wa Rukwa Bupe Mwakang’ata wakati akizungumza na wajasiliamali katika soko la sabasaba manispaa ya Sumbawanga.
Mwakang’ata amesema kuwa atahakikisha anawainuwa wanawake kiuchumi kwa kuwapa mikopo itakayowasaidia kuzungusha kwenye biashara zao na kisha kuzirudisha na wengine wakope.
“Natamani kuona wajasiliamali wanafanyabiashara zenye kuwapa faida na kuwa na mitaji inayoeleweka hivyo nitawakopesha ili wajiinue kiuchumi.”amesema Mwakang’ata
Amesema wajasiliamali wadogo wanaouza mboga mboga na matunda waungane ili wapate mikopo itakayowasaidia kukuza biashara zao.
Sambamba na hilo pia Mwakang’ata amewakabidhi wajasiliamali sh mill 1 kwa vikundi 10 sh laki Moja kwa Kila kikundi fedha ambazo zitasaidia kuongeza kipato.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya jamii manispaa ya Sumbawanga Noela Munisi amewataka wajasiliamali kuunda vikundi na kuvisajili jambo litakalo wasaidia kupata mikopo isiyokuwa na riba.
“Wajasiliamali wote hasa vijana undeni vikundi mje kusajili mikopo ipo kwa ajili yenu kazi kwenu kuchangamkia fursa hiyo”amefafanua Munisi.
Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi katibu wa soko la sabasaba Raymond Makelele amesema kuwa wajasiliamali hao wanakumbana na changamoto ya mtaji mdogo wa kuendeshea biashara zao hivyo wamemwomba awasaidie mikopo.
Katika hatua nyingine mwakang’ata amekabidhi mifuko 100 ya saruji na bando 4 za bati kwa ajili ya ujenzi wa jengo la UWT mkoa wa Rukwa.
Baadhi ya wajasiliamali waliopatiwa fedha hizo akiwemo Stephanie sumile amesema anamshukuru mbunge huyo kwa kuwawezesha wajasiliamali na amemtaka awe anawatembelea mara kwa mara.
Diwani wa viti maalumu Letisia Kipeta amewataka wajasiliamali kufanya biashara wakiwa na watoto wao wadogo na wasiwaache nyumbani kutokana na kukithiri kwa ukatili wa kijinsia.
“Msiwaache watoto nyumbani na hakikisheni mnawaogesha wenyewe na kuwakagua ili kuendelea kuwalinda watoto na vitendo vya ukatili”. amesema