Kassim Nyaki, NCAA
Wajumbe 85 kutoka nchi 15 za Afrika ambao ni Wajumbe Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika waliokuwa jijini Arusha kwenye mafunzo ya wajumbe wapya wa baraza hilo wametembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kustajabishwa na uzuri wa hifadhi hiyo iliyosheheni vivutio mbalimbali vya utalii.
Balozi wa Uganda Nchini Ethiopia Mhe. Rebecca Mugotengo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na malikale hali iliyowafanya wajumbe wa mkutano huo kuamua kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kabla ya kurudi kwenye nchi zao.
‘Wajumbe wa baraza baada ya kikao chetu Arusha tumechagua kuja Ngorongoro, tumekutana na watu wakarimu, Ngorongoro ni eneo lenye uoto wa asili lililotunzwa vizuri, mtawanyiko wa wanyamapori, ndege walioipamba hifadhi, Wanyama ni wengi siwezi hata kuzungumzia idadi yao, hali hii inawavutia wageni wengi kutembelea eneo hili” ameeleza Mhe. Rebecca.
Migel Mtutumu kutoka Nigeria ameeleza kuwa “lUNESCO haikukosea kuitambua hifadhi ya Ngorongoro kama eneo la urithi wa dunia kutokana na vivutio mbalimbali vilivyopo.
Amesema katika muda wa saa tatu waliotumia katika hifadhi hiyo wameona Wanyama mbalimbali ikiwepo Wanyama wakubwa watano ambao ni Faru, Chui, Simba, Nyati na tembo”
Naye balozi wa Botswana Nchini Ethiopia Mhe. Tibelelo Alfred amepongeza hifadhi ya Ngorongoro kuwa moja ya kivutio bora cha Utalii Afrika na kubainisha kuwa wananchi wa Afrika hawahitaji kupeleka fedha katika nchi za ulaya na kuacha vivutio adhimu ambavyo tunavyo katika bara la Afrika ambavyo vimekuwa kimbilio la wananchi wa mataifa mbalimbali.
Kiongozi wa Ujumbe huo ambaye ni Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Eugine Shio ameeleza kuwa wajumbe wa baraza hilo baada ya kumaliza programu ya mafunzo ya siku mbili jijini Arusha waliamua kuwaandalia ziara ya kutembelea hifadhi ya Ngorongoro waweze kujionea uzuri wa Ngorongoro na waliowengi imekuwa mara yao ya kwanza kuona idadi kubwa ya Wanyama wakiwa katika mazingira ya asili ikiwemo Wanyama wakubwa watano “Big 5” na kuahidi kurudi mara nyingine wakiwa na familia zao.