Mjumbe wa kamati ya utendaji Taifa ya Chama cha Walimu Tanzania Sabina Lipukila,akizungumza kwenye mkutano Mkuu wa Chama hicho Wilayani Tunduru.
Baadhi ya Walimu wilayani Tunduru,wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo Simon Chacha(hayupo pichani)wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma Simon Chacha,akizungumza na Walimu kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha wa pili kushoto,akiwa katika Picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania(CWT)Wilaya ya Tunduru na Mkoa wa Ruvuma baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika katika ukumbi wa Sky Way Tunduru.
Na Mwandishi Wetu,
Tunduru
CHAMA cha Walimu Tanzania(CWT) Mkoani Ruvuma,kimewataka viongozi wa ngazi ya matawi(Shule),kupanga muda wa kusikiliza kero za walimu kwenye maeneo yao na kuzipatia ufumbuzi ili kuongeza morali ya walimu kufundisha.
Wito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Taifa ya CWT Mkoa wa Ruvuma Sabina Lipukila wakati akiongea na wawakilishi wa walimu wa shule za msingi na sekondari wa wilaya ya Tunduru kwenye Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa kuwapata viongozi watakaokiongoza Chama hicho katika kipindi cha miaka mitano.
Lipukila alisema kuwa,kuna viongozi wanajifanya Miungu watu kwa kutosikiliza na kutatua changamoto za walimu hali inayosababisha baadhi ya walimu kukata tamaa na kukosa morali ya utendaji wa majukumu yao.
Amesisitiza suala la nidhamu,uwajibikaji na kufanya kazi kwa weledi ili kuwa mfano mzuri kwa walimu wa kawaida kuwa kada ya ualimu ni muhimu na ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa letu.
“Wapo walimu wanatembea umbali mrefu kwenda hadi makao makuu ya Halmashauri kwa ajili ya kufuata huduma kwa kuwa viongozi wao kwenye ngazi ya matawi(shule) wameshindwa kutatua na kuzipatia majawabu kero zao hali inayopelekea usumbufu mkubwa kwa walimu”alisema Lipukila.
Aliongeza,viongozi wa matawi na walimu wakuu wapo kwa ajili ya kuwasikiliza walimu na kuwasaidi kutatua kero zao ili waweze kujikita katika ufundishaji wa wanafunzi ,lakini walimu wanakatishwa tamaa na utendaji wa baadhi ya viongozi wasiojari maslahi ya wenzao.
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Simon Chacha,amewapongeza walimu kwa kazi nzuri ambayo imekuwa chachu ya mabadiliko katika Wilaya hiyo na Mkoa wa Ruvuma.
Chacha alisema,Serikali inawatambua na kuthamini kazi kubwa ya walimu na kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa kujituma na kwa weledi mkubwa ili kupata wasomi watakao kuwa viongoz bora wa Taifa letu.
“Hakuna Taifa lolote lililopiga hatua za maendeleo bila kuwa na walimu bora wanaozingatia sheria,weledi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri ya kitaaluma na kuondokana na matokeo mabaya,kazi mnazofanya walimu tunataka zitupe matokeo,jukumu lenu kubwa ni kuongeza ufaulu mashuleni kwa kutumia mbinu mbalimbali”alisema Chacha.
“Ufaulu mzuri unatokana kwa kufundisha sana darasani na hakuna njia nyingine katika hili,lazima mtumie nafasi zenu kufundisha kwa bidii”alisisitiza Mkuu wa wilaya”.
Katibu wa Chama cha Walimu wa Wilaya hiyo Mtamila Abdul alisema,wilaya ya Tunduru ina walimu 1,553 wakiwemo walimu wa shule za msingi,sekondari na chuo cha maendeleo ya jamii kati ya hao 1,268 ndiyo wanachama wa cha walimu Tanzania.
Mtamila alisema,katika kipindi cha mwezi Januari 2020 hadi Desemba 2024 Chama kimefanya kazi ya kutoa huduma kwa wanachama wake ikiwemo utetezi wa wanachama wenye kesi mahakamani,kutoa ushauri wa kisheria kwa masuala yanayohusu utumishi.
“Pia Chama kimetoa misaada ya fedha kwa wanachama wenye matatizo mbalimbalina kushirikiana mwajiri kuhakikisha walimu wenye sifa za kupandishwa vyeo wanapandishwa na kurekebishiwa mishahara na kuipongeza Serikali kupandisha vyeo vya na kutoa ajira kwa walimu”alisema Mtamila.